Mwendwa: Kenya haijakata tamaa, Tanzania ijiandae

Muktasari:

Kenya na Tanzania zimekutana mara 48, Kenya ikishinda mara 20 na Tanzania mara 14, huku sare ikiwa ni mara 14. Mara ya mwisho kuutana ilikuwa ni mwaka 2017, katika mashindano ya CECAFA, ambapo Kenya ilishinda 1-0.

Cairo, Misri. Rais wa shirikisho la soka la Kenya (FKF), Nick Mwendwa amesema Kenya haijakatishwa tamaa na matokeo ya mchezo wao wa kwanza, akitahadharisha kuwa mechi ya kesho Harambee Stars itashinda, hivyo wapinzani wao Tanzania wajiandae.

Mwendwa, ambaye yuko Cairo na Harambee Stars, alisema kila mtu alisikitishwa na matokeo ya mchezo ule, lakini hiyo haimanishi kuwa, kila timu itapata matokeo chanya kutoka kwa Stars, kwa sababu Kocha Sebastien Migne ameshafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza.

Kenya, iliyotandikwa 2-0 na Algeria, kesho Alhamisi, Juni 27, itaingia dimbani katika uwanja wa Jeshi, wakiwa na morali kubwa ya kupata, hasa kutokana na rekodi nzuri waliyonayo dhidi ya wapinzani wao, ambao wanakutana nao kwa mara ya kwanza, kwenye fainali hizi tangu mwaka 1969.

“Kusema ukweli, hatukufurahishwa na matokeo yale, tunaamini wakenya wametusamehe kwa kuwaangusha, lakini tunaahidi kutofanya makosa dhidi ya Tanzania. Hatujakatishwa tamaa na matokeo hayo ya Jumapili na Kocha amenihakikishia hilo,” alisema Mwendwa

Imani ya Mwendwa, inaungwa mkono na Kocha wa Kocha wa Harambee Stars, Mfaransa Sebastien Migne, Straika Michael Olunga na nahodha Victor Wanyama ambao wote wameonesha kuwa tayari kwa ajili ya mechi ya kesho, itakayopigwa kuanzia saa tano usiku.

Mechi ya keshi, itakuwa ya 49 kukutanisha timu hizi, ambapo mpaka sasa wameshakutana mara 48, Kenya ikishinda mara 20 na Tanzania mara 14, huku sare ikiwa ni mara 14. Mara ya mwisho kuutana ilikuwa ni mwaka 2017, katika mashindano ya CECAFA, ambapo Kenya ilishinda 1-0.