Makonda awatangazia vita Wakenya, Samatta ampa tano Magufuli

Muktasari:

Tanzania itaingia katika mchezo huo kwa lengo moja tu la kupata ushindi dhidi ya Kenya ili kurudisha matumaini yao katika Kundi C

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa kamati ya hamasa ya Taifa, Paul Makonda amesema kwa morali aliyoikuta kambi ya Taifa Stars hapo kesho Kenya hawatapona.

Makonda amesema morali ya wachezaji ipo juu baada ya kukutana nao na kuzungumza nao na sasa wako tayari kuipeperusha bendera ya Tanzania.

Makonda ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam amesema salamu za ujasiri kutoka kwa Rais John Magufuli zimewaongezea morali zaidi wachezaji hao kuelekea mchezo huo.

Akijibu maswali ya waandishi juu ya hali ya kambi ya timu hiyo alivyoikuta Makonda amesema kambi hiyo haiko sawa yamemshangaza na kuwataka watanzania kuungana kuiombea dua timu hiyo.

Aidha Makonda amesema licha ya Stars kupoteza mchezo wa kwanza matokeo hayo yasiwakatishe tamaa mashabiki na kuanza kuisema vibaya timu yao kwa kuwa bado iko vitani ikihitaji kumalizia mechi mbili zaidi.

Aidha Makonda amesema kipigo ambacho walikipata majirani Uganda kesho kitarudi kwa majirani wengine Kenya.

Naye nahodha wa Stars, Mbwana Samatta amesema salamu za Rais Magufuli zimewapa faraja na kwamba wako tayari kulipigania taifa.

Samatta amesema baada ya kupokea lawama kutoka kwa mashabiki lakini sasa wamerudi katika utulivu tayari kwa kupata ushindi kesho.

Makonda atua vyuoni kukusanya mashabiki

Mara baada kukuzungumza na wachezaji mwenyekiti wa kamati ya hamasa ya Taifa Stars, Makonda ameanza ziara ya kuzungukia vyuo vikubwa hapa Cairo kuwahamasisha mashabiki Watanzania kuja kwa wingi uwanjani.

Makonda ameanza kazi hiyo jioni hii hapa Cairo akitaka kuona Stars inashangiliwa kwa nguvu kesho.

Makonda alisema ameamua kufanya kazi hiyo akishirikiana na viongozi wenzake wa kamati na Rais wa TFF kuhakikisha Stars inapewa nguvu kesho.

 

Aidha Makonda amesema hata mashabiki waliobaki Tanzania nao wanatakiwa kuendelea kuiombea dua njema timu yao ipate ushindi katika mechi zake mbili zilizosalia.