Adidas yaikaba Manchester United kuhusu kumuuza Pogba

Muktasari:

Pogba alijiunga na Man United akitokea Juventus mwaka 2016 kwa ada ya Pauni 89 milioni na kuweka rekodi ya uhamisho duniani kwa kipindi hicho.

MANCHESTER, ENGLAND. Manchester United wapo kwenye presha kubwa ya kushinikizwa na wadhamini wao Adidas kuhusu kumbakiza kiungo Paul Pogba na kama wakimuuza basi wahakikishe wanasajili staa mwingine mwenye jina kubwa.
Kampuni hiyo ya Adidas imemwaga udhamini wa miaka 10 kwenye kikosi hicho cha Old Trafford wenye thamani ya Pauni 750 milioni kuanzia mwaka 2015 wakiamini kwamba timu hiyo itakuwa na mastaa wenye majina makubwa kwa ajili ya kuitangaza nembo yao.
Moja ya makubaliano katika dili hilo la Adidas, Man United ni kuhakikisha inawatumia mastaa wake katika matangazo yao kwenye masoko yao makubwa kama vile Asia, Ulaya na Marekani.
Na sasa Adidas wanaingia wasiwasi kwamba kumpoteza Pogba akinaswa na ama Real Madrid au Juventus zinazomtaka kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi basi jambo hilo litaifanya Man United kupoteza ubora wa nembo yake. Kipindi ambacho Adidas walikubali kumwaga udhamini huo wa wenye thamani ya Pauni 75 milioni kwa mwaka, staa wa Old Trafford alikuwa Wayne Rooney.
Hivyo, kama Pogba akiondoka katika dirisha hili, Man United watapaswa kupambana kwa nguvu zote kusajili mchezaji mwenye jina kubwa huku wakihakikisha kwamba kipa wao David de Gea haondoki kwa ajili ya kuimarisha zaidi nembo ya klabu hiyo. Kutokana na hilo ndio maana Man United inamthaminisha Pogba kuwa na thamani ya Pauni 160 milioni na wamemfanya kuwa balozi wa Adidas duniani.
Pogba alijiunga na Man United akitokea Juventus mwaka 2016 kwa ada ya Pauni 89 milioni na kuweka rekodi ya uhamisho duniani kwa kipindi hicho.