Kwako Kashasha: Hata Samatta atageuka kelvin Yondani Afcon

Sunday June 23 2019

Mwanaspoti, Kwako Kashasha, Michezo, Hata Samatta atageuka, kelvin Yondani Afcon, Tanzania, Senegal, Mwanasport

 

By Mwalimu Kashasha

KICHAPO cha bao 1-0 kutoka kwa Misri ilichopata Taifa Stars kilianza kutoa matumaini kwa mashabiki wake. Ilikuwa mechi ya kirafiki tu lakini Emmanuel Amunike, Kocha wa Taifa Stars alijua namna ya kucheza mechi kubwa kwa mara ya pili.
Mara ya kwanza ilikuwa katika pambano la kufuzu ugenini dhidi ya Uganda. Hatukutazama pambano la pili la kirafiki dhidi ya Zimbabwe. Vyovyote ilivyo nadhani alicheza kwa staili ile ile aliyotumia dhidi ya Uganda ugenini na kisha pambano la kirafiki Misri.
Taifa Stars haina ubavu wa kupishana na wakubwa wa kundi letu. Hatuna ubavu hata wa kupishana na majirani zetu Kenya. Staili yetu itakuwa ni kujaa katika boksi letu na kufanya mashambulizi ya kushtukiza.
Katika pambano dhidi ya Misri ungeweza kuona staa wa timu, Mbwana Samatta akirudi mpaka katika eneo lake kwa ajili ya kukaba kwa muda wote wa mchezo, Farid Mussa alikuwa anakaba kutokea kushoto na Simon Msuva ndiye ambaye walau alikuwa anaachwa kwa ajili ya mashambulizi ya kushtukiza.
Itabidi tukubali ukweli na tucheze hivi kama tunataka kuambulia chochote katika michuano hii. Inabidi twende na mifumo kama 4-5-1 au 3-5-1, lakini viungo watumike zaidi katika ukabaji na kusogea mbele kwa kasi wakipata mipira.
Tukijifanya wajuaji kama ambavyo mashabiki wengi wanataka timu yetu ishambulie wafurahie basi tutakwama. Tunaweza kuiahibika. Bado hatuna wachezaji wa kupishana na timu nyingi Ulaya. Huu ni ukweli ambao watu inabidi waambie.
Ili michuano hii tupate kitu, Samatta inabidi akabe kama Yondani, Farid akabe kama rafiki yangu Juma Nyosso na Bocco akabe kama Aggrey Morris. Ni njia muhimu kujenga uimara wa timu mbele ya safu ya ulinzi. Vinginevyo tutaaibika Cairo.
Kinachoshangaza mpaka sasa ni kitendo cha Amunike kumchezesha Bocco katika upande wa kushoto. Bocco hana mnyumbuliko wa kucheza pembeni. Anaweza kutokea pembeni akiwa maeneo ya mbele karibu na lango. Hawezi kucheza kwa kutokea nyuma kabisa. Hana kasi hiyo.
Ni bora Bocco asimame katikati halafu Msuva atokee kulia kwa sababu Msuva ana kasi. Lakini pia itatusaidia kupiga mipira mirefu ya juu eneo la katikati kwa Bocco kwa sababu ni mrefu na anaweza kusumbuana na mabeki katika eneo la mwisho.
Kama tutaweza kusafirisha mipira ya juu kwa haraka baada ya kuokoa basi Bocco anaweza kusababisha faulo au kupokea mipira vema kutokana na urefu wake. Hili ni jambo muhimu kwa kocha kulizingatia kwa sababu hivi ndivyo washambuliaji warefu wanavyotumika. Huwa hawachezi pembeni.
Katika kikosi ambacho Amunike alikuwa akichezea pale Nigeria mbele walikuwa wanamsimamisha Rashid Yekini mwenye umbo kubwa na akina Amunike walikuwa wanacheza pembeni kutokana na maumbo yao yalivyokuwa. Sijui kwanini Amunike hakumbuki hili.
Kila la kheri Stars. Ubora wao hautaamuliwa na uwezo wa Samatta au mchezaji mmoja mmoja. Utaamuliwa na jinsi ambavyo watacheza kitimu zaidi katika mechi zao tatu. Licha ya kufungwa bao 1-0 na Misri katika mechi ya kirafiki lakini walionyesha wanachoapswa kufanya.

Advertisement