Jose Mara agawa tuzo yake kwa Mjane wa Eric Cantona

Muktasari:

Cantona aliyekuwa mwanamuziki wa Mapacha Music Band alifariki katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Dawasco Tegeta jijini Dar es Salaam miezi sita iliyopita na kumuacha mke wake akiwa mjamzito.

Dar es Salaam. Mwanamuziki wa Mapacha Music Band, Jose mara ametoa zawadi ya Sh 340,000 kwa mke wa marehemu Eric Cantona baada ya wimbo wao wa 'Dunia Simama' kushinda katika shindano lililofanyika kwenye group la Whatsapp linaloitwa Dans Fans & Media Promo

Kundi hilo linaloundwa na wanamuziki, wanahabari na wadau wa muziki wa dance lilianzisha shindano hilo ikiwa ni kuwatia moyo wanamuziki hao na nyimbo zao zimekuwa zikishindanishwa na zawadi kutolewa.

Akizungumza wakati wa kupokea tuzo hiyo ya pesa taslimu Sh50,000, Jose alisema angependa pesa hizo pamoja na nyingine Sh290,000 ziende kwa mke wa marehemu Eric Cantona.

Cantona aliyekuwa mwanamuziki wa Mapacha Music Band alifariki katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Dawasco Tegeta jijini Dar es Salaam miezi sita iliyopita na kumuacha mke wake akiwa mjamzito.

Fedha hizo zilitolewa na kiongozi wa kundi hilo la Whatsapp, Mwandishi wa burudani wa magazeti ya Mwananchi na Mwanaspoti pamoja na Mwananchi Digital, Rhobi Chacha ikiwa ni pongezi kwa ushindi wao baada ya kuzimwaga bendi nyingine kama African Stars, Cp Academia, Bogoss Musica, Vijana Jazz, Double M Plus, Mapacha Og, Extra Bongo, T.O.T Plus, Washirika na Fm Academia.

Akizungumza kuhusu kundi hilo kutambua mchango wa wanamuziki wa dansi, Rhobi alisema katika shoo ya bendi hiyo iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Sun Sent uliopo Jet Lumo jijini Dar es Salaam, shindano hilo hufanyika mara kwa mara na awali walikuwa hawatoi zawadi na sasa wameona ili kuwatia moyo wanamuziki hao, watakuwa wakitoa zawadi kwa washindi kila baada ya Shindano.

"Sisi kama waandaaji, tunaipongeza bendi ya Mapacha Music Band ya Jose Mara na tunawakabidhi zawadi hii ya pesa Sh50,000 ili kuwatia moyo zaidi. Mimi na mwenzangu Tina Kinyonto tumejikusanya na kutoa zawadi hii na itakuwa ni endelevu kwa kila mpambano," alisema.