Obi Mikel hizi fainali zangu za mwisho Afcon

Muktasari:

 Baada ya miaka 13, Mikel mwenye umri wa miaka 32 ametangaza kustaafu kuichezea timu ya taifa ya Nigeria

Cairo, Misri. Nahodha wa timu ya taifa ya Nigeria, John Obi Mikel amesema fainali hizi za mataifa ya Afrika ‘AFCON’ nchini Misri 2019, zitakuwa fainali zake za mwisho kuichezea Super Eagles.

Mikel  mchezaji wa zamani wa Chelsea, aliyejiunga na  Middlesbrough ya daraja la kwanza  England amerejea tena na taifa lake Misri ambako alicheza kwa mara ya kwanza fainali za AFCON,  2006.

Baada ya miaka 13, Mikel mwenye umri wa miaka 32, alisema ni heshima kwake kuaga katika timu yake ya taifa ndani ya mji ule ule ambao alianza safari yake ya kuichezea Super Eagles katika fainali za AFCON ambazo huchezwa kila baada ya miaka miwili.

“Haitokuwa sehemu mbaya kwangu kumaliza, kabisa” alisema kiungo huyo muda mchache kabla ya mchezo wao wa ufunguzi wa fainali hizo ambapo walicheza dhidi ya Burundi kwenye uwanja wa Alexandria na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.

“Ninakumbuka mwaka 2006, nilikuwa kijana nikiwa na timu yangu ya taifa. Yalikuwa  mashindano yangu ya kwanza na yalikuwa bora kwa sababu tulimaliza katika nafasi ya tatu. Hili eneo (Misri) ni zuri kwangu,” aliongeza.

Mikel ni miongoni mwa wachezaji wa Kiafrika ambao wacheza soka la ushindani Ulaya kwa mafanikio, akiwa na Chelsea alikuwa sehemu ya kikosi kilichotwaa Ligi ya mabingwa Ulaya msimu wa 2011/12 pia uliofuata akatwa Europa Ligi, 2012/13.