Simba mpo! Okwi aanza Afcon kwa kishindo

Muktasari:

Uganda sasa inahitaji ushindi katika mchezo ujao dhidi ya Zimbabwe ili kufuzu kwa hatua ya 16 bora ya Fainali za Mataifa Afrika

Cairo, Misri. Mshambuliaji aliyetimka Simba, Emmanuel Okwi aliibuka shujaa kwa kuiwezesha timu yake ya taifa la Uganda ‘The Cranes’ kuibuka na ushindi wa mabao 2-0   katika mchezo wao wa kwanza wa fainali za mataifa ya Afrika dhidi ya DR Congo.

Uganda imekuwa timu ya kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kuibuka na ushindi katika fainali za Mataifa ya Afrika zinazoendelea kutimua vumbi nchini Misri.

Okwi aliifungia The Cranes bao la pili dakika ya 48 baada ya kuunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na kiungo, Faruku Miya alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo mara baada ya kumalizika.

Katika mchezo huo, Uganda walijipatia bao la kwanza kupitia kwa Patrick Kaddu alilifunga bao hilo kwa kichwa  kufuatia mpira wa adhabu uliochongwa na Faruku dakika ya 14.

 Uganda wanaongoza kundi A kutokana na idadi kubwa ya mabao waliyoipata mbele ya DR Congo, pamoja ua ushindi ambao pia waliupata Misri dhidi ya Zimbabwe watasalia katika nafasi ya pili.

Uganda wakiwa na Okwi, ambaye ni moja ya wachezaji muhimu katika kikosi chao, watacheza mchezo wao wa pili, Juni 26 dhidi ya Zimbabwe ambao walichapwa na Misri kwa bao 1-0.