Chirwa, Atta waonyeshwa mlango wa kutokea Azam FC

Muktasari:

Azam imefuzu kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la FA

Dar es Salaam. Uongozi wa klabu ya Azam FC umetangaza rasmi kuachana na mshambuliaji wake Obrey Chirwa baada ya kushindwa kufikia makubaliano ya kuongeza mkataba wake.

Mbali na Chirwa aliyejiunga na Azam FC dirisha dogo la usajili nyota wengine waliopewa mkono wa kwaheri ni pamoja na Joseph Kimwaga, Hassan Mwasapili, Enock Atta Agey, Twafazwa Kutinyu, Steven Kingu na Danny Lyanga.

Afisa habari wa klabu hiyo, Jaffar Idd alisema taarifa hizo zinaukweli wameachana na nyota hai baada ya kumaliza mikataba ndani ya klabu yao.

"Wamemaliza mkataba uongozi hawana mpango wa kuwaongeza wamewaacha wakajaribu maisha klabu nyingine na kuhusu Chirwa alikuwa katika mipango ya mwalimu lakini wameshindwana kutokana na mchezaji huyo kushindwa kufanya makubaliano."

"Tulikubaliana mara baada ya ligi kumalizika tukae meza moja kwaajili ya mazungumzo, lakini mchezaji huyo hakufanya ivyo aliondoka kwenda nchini kwao," alisema.

Jaffar alisema mara baada ya kuona mchezaji huyo haonyeshi ushirikiano katika suala la kuongezewa mkataba wameamua kumuacha huenda akawa na mipango yake mingine.