Kipute: Kenya, Tanzania zijipange kwa Simba wa Teranga

Muktasari:

Ratiba hiyo inaonyesha, Harambee Stars (Kenya) na wenzao Taifa Stars (Tanzania) chini ya kocha Mfaransa Sebastien Migne (Kenya) na Mnigeria Emmanuel Amunike (Tanzania), zitaanza kampeni zao Juni 23 katika dimba la Cairo na Juni 30 dhidi ya Algeria na Senegal.

HABARI ya mjini sasa hivi ni Fainali za Kombe la Dunia ya Wanawake zinazoendelea huko Ufaransa, Fainali za Copa America zinazokata mawimbi ya Brazil na Fainali za 32 za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) zitakazofanyika huko Misri kuanzia Juni 21.
Katika fainali Afcon, ambazo kwa mara ya kwanza katika historia ya soka la Afrika zitashirikisha mataifa 24 badala ya 16, huku pia zikifanyika katikati ya mwaka (Juni-Julai), badala ya Januari-Februari kama zamani, Tanzania na Kenya nazo ziko ndani unaambiwa!
Lakini pia Ukanda wa Afrika Mashariki ukiwa unawakilishwa na timu nne kwa mpigo, jambo ambalo halikuwahi kutokea kabla ya hapo, kwani Tanzania, Kenya, Burundi na Uganda zote zimefuzu fainali hizo zitakazoanza Jumamosi hii hadi Julai 19.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo inayoendeshwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Kenya iliyofuzu baada ya miaka 15 na Tanzania iliyorejea baada ya miaka 39 zimetupwa kwenye midomo ya Algeria na Senagal katika kundi C.
Ratiba hiyo inaonyesha, Harambee Stars (Kenya) na wenzao Taifa Stars (Tanzania) chini ya kocha Mfaransa Sebastien Migne (Kenya) na Mnigeria Emmanuel Amunike (Tanzania), zitaanza kampeni zao Juni 23 katika dimba la Cairo na Juni 30 dhidi ya Algeria na Senegal.
Wakati Tanzania ikianza na Senegal bila Sadio Mane katika mchezo utakaopigwa saa mbili usiku, Kenya wao watakutana uso kwa uso na Riyad Mahrez, saa mbili baadaye. Tanzania wana bahati ya kutokutana na Sadio Mane, ila wote wajipange kwa Simba hawa wa Teranga.

SADIO MANE
Ni mfumania nyavu, nahodha na mmoja wa wachezaji bora wa Afrika kwa sasa. Bila ubishi matumaini ya Senegal kutwaa ubingwa wa Afcon yako mikononi mwa Sadio Mane, na watakutana na Tanzania, lakini hatakuwepo.
Mane anaenda Misri akiwa na rekodi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku pia akiwa ni mfungaji bora wa Ligi Kuu ya England (EPL), akiwa na mabao 22 sawa na Mohammed Salah (Liverpool) na Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal.
Bila kutafuna maneno, mabeki wa Kenya ambao ni Musa Mohammed, Joseph Okumu, Joash Onyango, Philemon Otieno, Aboud Omar pamoja wenzao wa Tanzania kina Kelvin Yondani, Erasto Nyoni na Aggrey Moris wa sijui watatumia mbinu gani kumzuia asifanye mad hara? Tusubiri

ISMAILA SARR
Simba mwingine kutoka milima ya Teranga ambaye ni hatari kwa usalama wa Kenya na Tanzania, ni Straika wa Rennes, Ismaila Sarr. Kukosekana kwa Mane, katika mchezo wao na Taifa Stars, kunamaanisha kuwa Kocha Aliou Cisse atamtegemea kufanya makamuzi.
Msimu uliopita, Sarr alihusika katika mabao 24 ya Rennes, akifunga 13 na kuchangia mengine 11 katika michezo 50 aliyoingia dimbani. Kinda huyu mwenye umri wa miaka 21 ana kasi, uwezo mkubwa wa kupiga pasi na anapenda kuwafuata mabeki.

MBAYE NIANG
Ana miaka 24. Sambamba na Sarr, walikuwa moto wa kuotea mbali katika kikosi cha Rennes msimu uliopita. Mabao yake 14 yaliisaidia Les Rouges et Noir kutwaa taji la French Cup baada ya kuitandika PSG kwa penalti na robo fainali ya Europa League.
Mbaye Niang, ambaye yupo Rennes kwa mkopo akitokea Torino ana kasi, nguvu na akili. Inadaiwa kuwa klabu hiyo inataka kumbakisha. Huyu pia, atakuwa mwiba mkali kwa Kenya na Tanzania.

IDRISSA GUEYE
Kiungo huyu mwenye mapafu ya mbwa alikuwa na mchango mkubwa kwa Everton kwenye msimu uliopita wa EPL. Mchango wake ukatoa tuzo ya mchezaji bora wa msimu kwa klabu yake.
Alikuwa mchezaji wa pili aliyepiga ‘tackles’ na wa sita kwa wingi wa ‘interceptions’.
Tetesi za usajili zinasema kuwa yuko mbioni kuhama Goodison Park na kuelekea katika klabu kubwa za Ulaya. Anaelekea Misri akiwa na morali ya hali ya juu na atakuwa kikwazo kikubwa kwa viungo wa Tanzania na Kenya atakapokutana nao.

KALIDOU KOULIBALY
Anatajwa kuwa mmoja wa mabeki hatari na wanaowindwa kwa udi na uvumba duniani. Kila klabu inamtaka. Chelsea, Arsenal na Manchester United zote zinaumiza kichwa kwa ajili yake. Mashetani Wekundu wanadaiwa kuwa katika nafasi nzuri ya kumnyakua.
Nani asiyeujua ubabe na umakini wa miguu ya Kalidou Koulibaly? . Sijui Mbwana Samatta na Michael Olunga watatumia njia gani kumpita?
Beki huyu wa Napoli, mwenye umri wa miaka 27 naye atakuwa moto wa kuotea mbali. Hata hivyo, iwavyo vyovyote, Tanzania na Kenya zinapaswa kujipanga vilivyo. Tukutane Misri!