Hisia zangu: Kevin John, miluzi mingi isiyo na sababu

Muktasari:

Rafiki mmoja wakala kutoka Afrika Magharibi majuzi alitua katika michuano ya Afcon na kudai anaweza kumpeleka Kevin John katika klabu ya Anderlecht lakini hawezi kufanya hivyo kwa sababu Kevin ana wakala wake

Wote tunakubaliana kwamba Kevin John ‘Mbappe’ ni Mbwana Samatta ajaye. Lakini naanza kupata hofu ya hatima yake. Kuna miluzi mingi kando yake. Inaonekana karibu klabu zote Ulaya zinamtaka yeye. Sifa zake ni nyingi.
Niliwahi kusafiri naye kutoka Lesotho mpaka Johannesburg, Afrika Kusini akinisimulia jinsi alivyowatesa wazungu wakati alipoenda kufanyiwa majaribio Denmark. Wakati huo alikuwa Afrika Kusini kufanya majaribio na Ajax Cape Town.
Akaniambia kwamba mpango mzima ulikuwa ni wa yeye kwenda Ajax Amsterdam kupitia tawi lao la Ajax Cape Town pale Afrika Kusini. Mpaka leo kimya. Sijui mpango umekufa au Ajax wamezidiwa kete na klabu nyingine.
Hapohapo pia akaniambia kuna klabu za Italia kama vile Lazio zinamtaka. Niliporudi kukawa na hadithi nyingi kuhusu Kevin. Mtu mmoja akaniambia anatakiwa na klabu za Ubelgiji, mwingine akaniambia anatakiwa na wakala wa Gareth Bale.
Nilipoenda Genk kumtembelea Mbwana Samatta akaniambia kuna mchezaji mwenzake wa zamani wa Genk aliwahi kumpigia simu kumuulizia kama anamfahamu Kevin John. Wakala wa huyo mchezaji alikuwa anamtaka Kevin.
Rafiki mmoja wakala kutoka Afrika Magharibi majuzi alitua katika michuano ya Afcon na kudai anaweza kumpeleka Kevin John katika klabu ya Anderlecht lakini hawezi kufanya hivyo kwa sababu Kevin ana wakala wake.
Lakini nikawahi kuambiwa kwamba wakala wake pamoja na mdau mmoja wa soka wanamfanyia mpango akacheze Marekani. Siamini sana katika nchi inayoitwa Marekani linapokuja suala la soka la kulipwa. Pesa ipo lakini Ulaya kunamfaa zaidi mchezaji wa aina yake.
Majuzi nikasikia stori nyingine kwamba kuna vigogo nchini wamejaribu kumuunganisha Kevin na klabu ya Porto ya Ureno kupitia kwa bosi mmoja anayejuana na watu wa Porto pamoja na klabu kadhaa za nchini Ureno.
Na sasa kila siku utasikia Kevin akihusishwa na Ulaya. Hata hivyo, bado yupo hapahapa tu. Uwanjani ni simba anayetisha. Ana kipaji cha kuziona nyavu na kila siku anaimarika. Wakati wa michuano ya Afcon, Serengeti Boys ilifanya ovyo lakini ungeweza kuona kipaji chake kikubwa.
Nje ya uwanja, Kevin amegeuka kuwa simba wa karatasi. Jina lake linatisha zaidi katika mipango ya hapa na pale lakini ukweli ni kwamba hatujui hatima ya maendeleo yake kuhusu kwenda kucheza nje ya nchi. Tunasikia mipango zaidi.
Kevin alihitajika kwenda nje sasa na kukulia katika mifumo zaidi ya kisoka. Haendi katika kikosi cha kwanza, anapaswa kwenda katika timu za vijana. Anahitaji kwenda mahala, kutulia na kuzingatia mafunzo. Asibakie katika danadana zetu za kutakiwa kila mahala.
Hatimaye hata uvumi wa hatima yake mwenyewe unaweza kumuharibu kisaikolojia. Kwa wenzetu mchezaji hapaswi kuwa katika uvumi wa usajili kwa muda mrefu. Anahitajika kuwepo mara tulivu na kuifanya kazi yake. Habari ya mara leo Ajax, kesho Ulaya, keshokutwa Marekani haina mpango.
Inakera unapotembea mitaani na mashabiki wakakuuliza hatima ya Kevin. Jibu lake ni kwamba ‘Sijui. Nadhani ana meneja wake au wakala wake anayemshughulikia jambo lake’. Jambo gani? ni jibu ambalo watu wa soka wote hatufahamu.
Katika hili pia kuna uwezekano mkubwa Kevin akaharibika na kujiona staa zaidi ya Mbwana Samatta kwa sababu anauliziwa na kila mtu kuhusu uwezekano wa yeye kwenda Ulaya. Inawezekana hata meneja wake anamuona Kevin ni kama Samatta tu. Hata hivyo, hajafika huko na anahitaji mwongozo sahihi kuweza kufika huko. Walio karibu naye wasimdanganye.
Kwa sasa hakuna timu ambayo itamnunua Kevin kwa pesa nyingi au kumlipa pesa nyingi. Kilichopo ni wazi kwamba baada ya miaka minne Kevin anaweza kulipwa pesa nyingi kwa klabu atakayochezea, huku klabu yake ya sasa anayochezea nchini ikilipwa pesa nyingi kama akiingia mkataba wake wa kwanza wa kulipwa nje, au akiuzwa kwenda kwingineko. Soka la kulipwa ni mchakato. Hata Samatta hakuwa Samatta ndani ya wiki mbili.
Pamoja na yote haya ambayo kwangu nayaona kama danadana kuhusu suala lake la kwenda nje, kitu ambacho kinanifurahisha ni jinsi ambavyo jina la Kevin linahusishwa kwenda nje tu. Huu ni mwanzo mzuri. Kwa sasa wachezaji wetu wa timu za vijana wameanza kwenda nje moja kwa moja bila ya kuhusishwa na zile timu pacha za Kariakoo. Ni jambo jema.
Tayari tuna Ali Ng’anzi anayecheza soka la kulipwa Marekani, kuna Nickson Kibabage aliyekwenda Klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco na kusaini mkataba wa miaka minne wiki iliyopita.
 Wote hawa hawakuwa na ndoto za kupita katika klabu pacha za Kariakoo kwa sababu tuna vijana wengi ambao wanajiona kuwa kama Mbwana Samatta au Simon Msuva ndani ya miaka michache ijayo.