Mshambuliaji Oliech yeye ni Gor Mahia tu

Muktasari:

Oliech aliyetesa sana na Harambee Stars, pia alipokuwa akicheza soka lake la kulipwa ligi kuu ya Ufaransa kwa zaidi ya mwongo, alikuwa amestaafu soka. Hata hivyo baada ya miaka miwili nje, alirejea msimu uliopita kwa kujiunga na Gor kwa mkataba wa miaka miwili.

Nairobi. Klabu ya Gor Mahia imekanunusha tetesi straika mkongwe Dennis Oliech waliyemsajili mwanzoni mwa msimu uliopita ni mmoja wa wachezaji wanaopania kuchuja kabla ya msimu mpya kuanza.
Oliech aliyetesa sana na Harambee Stars, pia alipokuwa akicheza soka lake la kulipwa ligi kuu ya Ufaransa kwa zaidi ya mwongo, alikuwa amestaafu soka. Hata hivyo baada ya miaka miwili nje, alirejea msimu uliopita kwa kujiunga na Gor kwa mkataba wa miaka miwili.
Japo aliahidi kutesa kwenye msimu wake wa kwanza, Oliech (34) hakuweza kufanya chochote kikubwa.
Baada ya msimu kumalizika kukaibuka na taarifa uongozi unawazia kumwangushia shoka baada ya kushindwa kuridhishwa na kiwango chake kinyume na ilivyotarajiwa.
Oliech alimaliza msimu uliopita vibaya kwa kuvunjika mkono kwenye mechi yao dhidi ya Western Stima mwezi Mei na ili aweze kupona vyema atahitaji angalau miezi mitano, kipindi ambacho ni kirefu sana kwenye soka.
Hii ndio sababu ya kuwepo kwa tetesi hizo Oliech na wachezaji wengine waliokosa kufurahisha, watatupwa nje.
Hata hivyo kulingana na Ofisa mkuu Mtendaji wa Gor, Lordvick Aduda, uongozi wa klabu hauna mpango huo kabisa.
“Sio kawaida yetu kumtema mchezaji anapokuwa majeruhi. Mliona tulivyofanya na Wellington Ochieng, pia Karim Nizigiyimana. Kufikia wakati tunamwachia Karim, alikuwa amepona vizuri na kuwa fiti. Oliech vile vile tutamwangali hadi atakapopona vizuri. Anahitaji miezi tano au sita hivi na tutakuwa naye hatua kwa hatua,” Kasema Aduda.
Oliechi akiwa ameumia na straika Mrwanda Jacques Tuyisenge akiwa ameshaondoka, Gor wana kibarua cha kumsaka straika wa kusaidiana na Nicholas Kipkurui, fowadi wa pekee aliyesalia kikosini humo akiwa fiti.