Sokoni fungua pochi ujibebee hawa

Muktasari:

Ndivyo linavyobainisha soko lao. Bei yao huko sokoni usipime. Bei ya Hazard sokoni, inadaiwa kuwa ni Pauni 107.2 milioni, hivyo kiwango walichotoa Los Blancos hawajapotea sana, ndio bei yake.

London, England. KIZURI gharama jombaa. Ndiyo hiyo, usione tu kizuri, kukipata ugharimie. Real Madrid imeshamnasa Eden Hazard, bonge la mchezaji. Ni mzuri hasa, lakini unajua, imewatoka kiasi gani? Pauni 150 milioni.
Kwanza imetanguliza Pauni 130 milioni, kisha hizo nyingine zitalipwa kidogo kutokana na Hazard akifikia baadhi ya mambo huko Santiago Bernabeu. Ni hivyo, kumpata mchezaji mzuri kunahitaji pesa nyingi.
Wachezaji wote unawajua wewe kuanzia Kylian Mbappe, Neymar, Paul Pogba, Hazard mwenyewe, Mohamed Salah, Raheem Sterling, Sadio Mane, Marcus Rashford, Harry Kane, Virgil van Dijk wote hao ukiwagusa hao, pesa ndefu lazima ikutoke.
Ndivyo linavyobainisha soko lao. Bei yao huko sokoni usipime. Bei ya Hazard sokoni, inadaiwa kuwa ni Pauni 107.2 milioni, hivyo kiwango walichotoa Los Blancos hawajapotea sana, ndio bei yake.
Mtandao unaohusiana na kutoa tathmini ya thamani za wachezaji sokoni, CIES Football Observatory, ambao umekuwa ukitoa thamani za wachezaji kila mwaka tangu 2013, umeibuka na orodha ya wachezaji ambao ukitaka huduma zao, usikurupuke tu, ujipange kwelikweli. Uwe na hela.
Kwenye orodha yao hiyo, supastaa Mbappe hagusiki, ukimtaka bei yake sokoni ni Pauni 223.8 milioni. Kama huna mkwanja unaoanzia kiasi hicho, kaa pembeni.
Supastaa wa Liverpoo, Salah anafuatia kwa kuwa na thamani kubwa, ukimtaka, basi jiandae na mkwanja unaoanzia Pauni 195 milioni, kisha anakuja staa wa Manchester City, Raheem Sterling, ambaye huko sokoni kibao chake kinachomeka Pauni 184.6 milioni.
Lionel Messi wa Barcelona yupo kwenye namba nne, kibao chake cha bei kinasema Pauni 148.7 milioni kama unahitaji huduma yake kwa bei ya sokoni, wakati Tano Bora inakamilishwa na kinda wa Kingereza, Jadon Sancho anayekipiga Borussia Dortmund, amening’inizwa bei ya Pauni 141.6 milioni huko sokoni kama utamtaka.
Wanaofuatia, yupo Sadio Mane wa Liverpool, ambaye kibao chake kinasema Pauni 140.2 milioni, wakati Kane wa Tottenham Hotspur bei yake ya sokoni ni Pauni 137.9 milioni, kisha Roberto Firmino wa Liverpool Pauni 128.13 milioni, Antoine Griezmann ubao wake wa bei unaonyesha Pauni 127.7 milioni na anayekamilisha 10 bora ni staa wa Man City, Leroy Sane, ambaye ubao wake wa bei, unasema thamani yake ni Pauni 121.8 milioni.
Cheki, vichwa vyote hivyo makini ndio maana bei yao ya sokoni imechangamka pia.
Wanaofuata kwa kuwa na bei kubwa sokoni ni Bernardo Silva, Pauni 121.6 milioni, Gabriel Jesus (Pauni 116 milioni), Trent Alexander-Arnold (Pauni 115.6 milioni), Philippe Coutinho (Pauni 114.9 milioni), Romelu Lukaku (Pauni 111.2 milioni), Paul Pogba (Pauni 111.1 milioni na staa wa PSG, Neymar, ambaye ubao wake wa bei huko sokoni kwa sasa unasema anauzwa Pauni 110.8 milioni.
Rashford ubao wake unasomeka Pauni 109.7 milioni, Hazard (Pauni 107.2 milioni), Cristiano Ronaldo (Pauni 104.94 milioni), Ousmane Dembele (Pauni 104 milioni), Virgil van Dijk (Pauni 99.6 milioni), Paulo Dybala (Pauni 96.1 milioni), Alisson Becker (Pauni 95.5 milioni), Aymeric Laporte (Pauni 93.6 milioni), Ederson (Pauni 91.5 milioni), Dele Alli (Pauni 91 milioni), Richarlison (Pauni 87.6 milioni), Son Heung-min (Pauni 86.3 milioni) na kipa wa Barcelona, Marc-Andre ter Stegen anakamilisha 30 bora ya wenye thamani kubwa huko sokoni, ambapo kipa huyo anaripotiwa bei yake ya sokoni ni Pauni 84.5 milioni.
Kwenye orodha hiyo ya masupastaa 30 wa maana wenye bei zilizokaa sawa huko sokoni, unaweza kutengeneza vikosi vya kwanza kibao, kikiwamo hiki chenye thamani ya Pauni 1.429 bilioni, ambacho kitajumuisha mastaa tisa wa Ligi Kuu England na wawili wengine, mmoja kutoka Ufaransa, supastaa anayeongoza kwa bei mbaya sokoni, Mbappe na kiungo wa Barcelona, Philippe Coutinho.
Mfano wa kikosi hicho, golini anaweza kusimama kipa Alisson, kisha mabeki wake, kulia ni Alexander-Arnold, kushoto Robertson na kati ni Van Dijk na Laporte. Kwenye kiungo mastaa wake watatu watakuwa Coutinho, Pogba na Bernardo, wakati fowadi itakuwa na Mo Salah, Sterling na Mbappe.
Vyovyote utakavyotaka kufanya, ukiamua kusajili wachezaji kutoka kwenye orodha na kutengeneza kikosi kimoja matata, basi thamani ya kikosi hicho lazima hesabu zake zitaanzia kwenye Pauni Bilioni Moja na kuendelea. Team Pesa!