Ukweli Ndivyo Ulivyo! Acheni tu kina Ndemla wachekwe na kina Okwi

MAISHA yana changamoto nyingi na ili uweze kumudu eneo lako, lazima juhudi binafsi, maarifa, nidhamu pamoja na elimu ni vitu muhimu unavyohitaji kukubeba.
Unaweza ukalazimika kuwa na vyote kwa pamoja ili kuwa bora zaidi na wakati mwingine ukatumia kimojawapo vizuri ili kwenda mbali zaidi.
Vitu hivyo tu ndivyo vinavyoweza kukufanya utofautiane na wengine unaoshindana nao iwe kwenye biashara, kazi au maisha ya kawaida. Juhudi binafsi zinampa binadamu husika njia mbadala ya kupambana na uhalisia hata kama itatokea amepishana na elimu.
Hilo unaweza kulihamishia hata kwenye soka letu. Hakuna ubishi kuna tofauti kubwa kati ya wachezaji wa Tanzania na wale wa nchi nyingine za Afrika Mashariki. Wachezaji wetu kwa mtu ambaye hawajui anaweza kudhani ni aina fulani ya nyota wenye uwezo mkubwa sana wa kiuchumi au ambao wameridhika sana, kumbe wala sio.
Hawa kina Ibrahim Ajibu, Said Ndemla, Jonas Mkude, Salum Abubakar na wengineo, wanazidiwa sana maarifa ya ndani na nje ya uwanja na wachezaji wengine kutoka ukanda huu tu, hapo sijawaweka wale wanaotoka nje ya Afrika Mashariki.
Inawezekana mashabiki wa soka hawajui, ila ukweli wachezaji wengi wa Tanzania hawana wivu wa maendeleo, hawaweki juhudi kwenye kutafuta njia mbadala ya maisha ya soka kama ilivyo kwa wenzetu na vilevile ukiingia ndani sana unaweza kugundua hawapendani. Hawajadiliani. Chukulia mfano mdogo tu maisha ya wachezaji wa Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi ambao ndio wengi wanacheza nje. Wachezaji hao wana wivu mkubwa wa maendeleo na wanabebana, mtu akitoka nje anapambana kupiga hatua zaidi ya mwenzie ili apate masilahi mazuri na kujenga jina na ni mara chache sana kusikia wamerudi nyuma.
Wanajua nini maana ya thamani ya Dola na hata mchezaji akihisi anachemka, huku utasikia ameibukia kule lakini huwezi kusikia anatamani kurudi nyumbani kama nyota wetu wanaokata dili za maana nje ili wazichezee Simba na Yanga. Huwezi kusikia nyota wa nchi jirani wakipigana vikumbo kurudi nyumbani ili kukipiga Gor Mahia na AFC Leopards ama  SC Villa na URA kama sio Rayon Sport na APR.
Bahati mbaya nyota wetu wakienda kidogo hata hapo Zambia kama sio Afrika Kusini, Kenya ama Ulaya wanaanza kulialia na kukimbilia kurudi Dar es Salaam kutafuta sifa za Uwanja wa Taifa. Mara kadhaa tumekuwa tukiona nyota wa nchi jirani kama kina Emmanuel Okwi ama tu Meddie Kagere wanavyokomaa nje ya nchi yao, wakiwa wala hawana hamu ya kurejea kwao. Haruna Niyonzima ana zaidi ya miaka mitano anacheza Tanzania, anaranda mitaa ya Kariakoo akitoka Yanga anaenda Simba. APR alikotoka milango i wazi kwake, lakini anakomaa Tanzania.
Donald Ngoma, Obrey Chirwa tangu watue Tanzania kama ilivyo kwa Amissi Tambwe wala hawana mzuka wa kurudi kwao, licha ya kutambua hawavumi kama enzi walivyokuja. Wanakomaa kwa sababu wanatafuta fedha. Wachezaji wazawa, uvumilivu na ubishi wa aina hiyo hawana. Ndio maana tulimwona Juma Liuzio ‘Ndanda’ akirejea kutoka Zambia. Tulimwona Haruna Moshi ‘Boban’ akichomoka kule Sweden ili aje kukipiga Friends Rangers kabla ya kutua African Lyon na sasa Yanga. Pia ndivyo tuliona kwa Shomary Kapombe aliyetoka Cannes ya Ufaransa ili arudi nyumbani.
Ndivyo ambavyo tunamwona Shaaban Idd Chilunda amerejesha majeshi na pengine sio ajabu kusikia Rashid Mandawa naye akirudi nyumbani baada ya kukipiga pale Botswana. Kwa wazawa ni jambo la kawaida kwenda nje na kurudi fasta nchini, labda ukiwaondoa Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ambao kuna wakati huwadhania labda si Watanzania.
Miaka michache iliyopita tuliona Okwi aliyekuwa amesajiliwa na klabu ya Sønderjyske ya Denmark, ambako hakuwa na namba, lakini aliendelea kukomaa kabla ya kuamua kurejea Msimbazi na kutengeneza ufalme flani hivi uliokuja kutibuliwa na Kagere.
Kwa sasa mkataba wake Msimbazi umeisha, lakini hutaona dalili za kurudi kwao. Utaona anasita kurudi nyuma kutokana na uelewa wake mpana, malengo yake pamoja na wivu wa maendeleo. Anaona akirudi nyuma kuna kitu fulani atapoteza, anaona kwa kuendelea kukaa kule kuna njia nyingine inaweza ikafunguka siku yoyote. Hayo ni mambo ambayo mswahili hawezi kuyafikiria. Kwa Mzawa ungekuta amesharudi Dar es Salaam tena anasema; “Asante Mungu kwa kunirudisha nyumbani.”
Hata hawa nyota wetu ambao wamekuwa wakiwatoa povu wachambuzi na mashabiki wa soka kwa kukataa kwenda nje, wangekuwa na mzuka kama huo wala tusingechoshana kuwajadili. Wangekuwa wakipepea anga kwa anga kama Samatta ama Ulimwengu. Samatta katoka Simba katimkia TP Mazembe ya DR Congo na mara shaa, katua Genk ya Ubelgiji na sasa nawaza kutimba England. Ulimwengu naye vivyo hivyo, hafikirii kurudi nyumbani, japo dirisha dogo la usajili kuna watu walimvumisha ametua Msimbazi, lakini aliwakacha Al Hilal ya Sudan na kutua JS Saoura ya Algeria. Ndivyo inavyotakiwa.