Lampard apewa kiki Chelsea

Monday June 17 2019

 

LONDON, ENGLAND. KOCHA wa zamani wa West Ham United, Harry Redknapp amesema Frank Lampard atakwenda kumaliza ubabe wa wachezaji huko Chelsea.
Ubabe wa wachezaji kwenye kikosi cha Chelsea umedaiwa kuwagharimu makocha wengi sana huko Stamford Bridge, lakini Redknapp, 72, anaamini kwamba ugwiji wa Lampard kwenye timu hiyo utakwenda kumaliza nguvu ya wachezaji katika timu hiyo.
Lampard anatajwa kwamba huenda akaachana na Derby County na kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa Chelsea baada ya Maurizio Sarri kudaiwa kwamba atatimkia zake Juventus.
Redknapp alisema: “Atakuwa na mamlaka kamili. Hawezi kunyamazia upuuzi. Eden Hazard ameondoka na alikuwa mchezaji mahiri. Hakutakuwa na utovu wa nidhamu kwa wachezaji wengine wote waliobaki, lakini hakuna hata mchezaji mmoja ambaye atamtazama Frank na kusema 'mimi ni mkubwa, ni mchezaji mkubwa'.
“Amekuwa mchezaji bora Chelsea kuliko yeyote aliyewahi kutokea kwenye timu hiyo. Hilo tu linampa mwanzo mzuri. Hakuna mchezaji yeyote hapo ambayo atashindwa kummudu."
Lampard ameshindwa kuipandisha Derby Ligi Kuu England baada ya kupigwa na Aston Villa katika mechi za mchujo, lakini Chelsea wanadaiwa kwamba wanataka huduma yake licha ya ripoti za hivi karibuni kudai Derby nao wanamwaandalia mkataba mpya. Chelsea kumpata Lampard itabidi iwalipe Derby fidia ya Pauni 4 milioni.

Advertisement