Real Madrid kumtoa Bale kwa mkopo Bayern

Muktasari:

Zinedine Zidane alishindwa kujizuia wiki chache zilizopita kuwa hana mipango ya kuendelea kufanya kazi na winga huyo wa zamani wa Tottenham

Madrid, Hispania. Real Madrid wanaangalia uwezekano wa kumtoa kwa mkopo Gareth Bale kipindi hiki cha usajili kwa kujiunga na miamba ya soka la Ujerumani, Bayern Munich.

Wakati Manchester United wametajwa kugomea usajili wa nyota huyo wa kimataifa wa Wales, mabingwa wa Ligi ya Ujerumani wanatajwa kuwa wapo tayari kulipa nusu ya mshahara wake.

Bale amekuwa akivuta Paund 350,000 kwa wiki baada ya kukatwa kodi hivyo wanatajwa kukubali  kusaidiana na Real Madrid katika malipo ya mshahara wake huo ili akazibe mapengo  yaliyoachwa  na  Arjen Robben  na  Franck Ribery, walioondoka  mwishoni mwa msimu huu.

Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane alishindwa kujizuia wiki chache zilizopita kuwa hana mipango ya kuendelea kufanya kazi na winga huyo wa zamani wa Tottenham.

Real Madrid   wako tayari kumuachia Bale ili  kuwa na uwiano mzuri wa mapatano na matumizi yao kwenye usajili ambao umekuwa ukifuatilia kwa ukaribu na shirikisho la soka duniani (FIFA) kupitia kanuni zao za udhibiti wa matumizi makubwa ya fedha zilizonje ya utaratibu rasmi wa uzalishaji wa  klabu.

Matajiri hao wa Madrid, tayari wamewanasa wachezaji watatu kipindi hiki cha usajili ambao ni Eden Hazard, Luka Jovic  na   Ferland Mendy.