Sarri aondoka Chelsea rasmi, atue Juventus

Muktasari:

Sarri amedumu kwenye kikosi cha Chelsea kwa miezi 11 huko Stamford Bridge, akiwaongoza kubeba ubingwa wa Europa Ligi na kuwarudisha kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao

London, England. Hatimaye Chelsea imethibitisha kocha wake Maurizio Sarri ameondoka katika timu hiyo akienda zake kuinoa Juventus.

Juventus, wamemtangaza Sarri kuwa kocha wao mpya, akisaini mkataba wa miaka mitatu wa kuinoa timu hiyo akichukua mikoba ya Max Allegri, aliyeachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu uliopita.

Sarri amedumu kwenye kikosi cha Chelsea kwa miezi 11 huko Stamford Bridge, akiwaongoza kubeba ubingwa wa Europa Ligi na kuwarudisha kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kumaliza nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita.

Sarri, ambaye alikuwa kocha wa Napoli huko nyuma aliripotiwa kutaka kuachana na Chelsea muda mfupi tu baada ya kuifunga Arsenal kwenye fainali ya Europa League, akidai kwamba anataka kurudi kwao Italia kuwalea wazazi wake ambao ni wazee zaidi. Sarri mwenyewe ana umri wa miaka 60.

Mkurugenzi wa Chelsea, Marina Granovskaia alisema: "Kwenye mazungumzo tuliyofanya baada ya fainali ya Europa Ligi, Maurizio alionyesha wazi dhamira yake ya kutaka kurudi kwao, akisema sababu zinazomrudisha kufanya kazi Italia ni muhimu zaidi.

"Aliamini ni jambo muhimu kuwa karibu na familia yake kwa ajili ya ustawi wa wazazi wake wazee sana ambao anadhani ni muhimu akaishi nao karibu kwa kipindi hiki.

"Maurizio anaondoka Chelsea tukimshukuru sana kwa yote aliyofanya yeye na wasaidizi wake kwa kipindi chote cha msimu aliokuwa hapa kama kocha wetu mkuu na kushinda taji la Europa League, alitufikisha fainali ya kombe la ndani na kumaliza nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu England.

"Tunapenda pia kumpongeza kwa kupata kazi kubwa kabisa huko kwenye Serie A na tunamtakia kila la heri."