VIDEO: Yanga kweli kubwa kuliko yaipora Simba mchana nyavu hatari

Muktasari:

Yanga imetumia saa 12 kuonyesha jeuri nzito ya nguvu ya wanachama na wadau wake baada ya kukusanya fedha taslimu na ahadi kwa zaidi ya Sh900 milioni, lakini kubwa kuliko ni kumtambulisha staa mwingine mkali wa kufunga ndani ya ukumbi

Dar es Salaam. UTABISHA nini sasa! Yanga kweli ni kubwa kuliko na jana Jumamosi ilidhihirisha wakati walipofanya hafla yao ya harambee ya kuchangishana fedha, pia ilitambulisha nyota wake wapya akiwamo mchana nyavu waliyempora kutoka kwa watani wao Simba.
Katika hafla hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam zaidi ya nusu bilioni zilikusanywa ikiwamo fedha taslim na ahadi kutoka kwa wanayanga, huku Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda akiahidi kutoa uwanja eneo la Kigamboni.
Ipo hivi. Yanga imetumia saa 12 kuonyesha jeuri nzito ya nguvu ya wanachama na wadau wake baada ya kukusanya fedha taslimu na ahadi kwa zaidi ya Sh900 milioni, lakini kubwa kuliko ni kumtambulisha staa mwingine mkali wa kufunga ndani ya ukumbi. Hafla iliyofanyika jana ni ya kukusanya michango lengo lilikuwa wakihitaji kupata Sh1.5 bilioni kukisuka kikosi chao kwa msimu ujao wa ligi.
Mkutano ulivyoanza katika hafla hiyo iliyoanza saa 4:00 asubuhi iliyokuwa na shangwe wakati wote mpaka ilipotimu saa 6:20  mchana tayari ukumbi wa Diamond Jubilee ulikuwa umeshajaa na kubaki meza chache za wageni maalumu.

BALINYA         ATAMBULISHWA
Balaa la shangwe la Yanga lilianza pale Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebela alipokuwa akitambulisha watu muhimu waliopo katika ukumbi huo.
Mwakalebela aliwainua wanachama na mashabiki wa Yanga baada ya kumtambulisha mshambuliaji mpya, Juma Balinya kutoka Uganda aliyewasili alfajiri ya jana.
Balinya ndiye Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Uganda msimu huu akiichezea Polisi Uganda na alikuwa akihusishwa kusajiliwa na Simba baada ya Meneja wa Meddie Kagere, Patrick Gakumba aliwapelekea mabosi wa Msimbazi jina lake na wengine wawili ili wasajiliwe.
Mganda huyo anayemudu kiungo mshambuliaji alisainishwa mkataba wa miaka miwili mara baada ya kuwasili na kuwa mchezaji wa nane mpya kusajiliwa msimu huu. Katika utambulisho huo Mwakalebela alisema wakati Balinya akitangazwa amesajiliwa na Simba na gazeti moja la michezo (sio kutoka kampuni ya Mwananchi) mshambuliaji huyo ataichezea Yanga. “Kuna gazeti limeandika leo (jana) Balinya amesaini upande wa pili miaka miwili sasa leo nawaambia Wanayanga Balinya yupo hapa ndani na ameshasajiliwa kwa miaka miwili naomba aje awasalimie,” alisema Mwakalebela huku salamu hizo ziliufanya ukumbi ulipuke kwa shangwe.
Mwanaspoti lilikuwa linafahamu, Yanga ilikuwa ikimvizia mshambuliaji huyo sawa na Simba kutokana na umakini wake wa kujiridhisha katika taarifa.
Mbali na Balinya pia Mwakalebela alimtambulisha kiungo wao mpya Mzanzibar Abdulaziz Makame ambaye alikuwa ndani ya ukumbi huo sambamba na mastaa wengine ambao wameshawasajili wakiwemo Issa Bigirimana, Patrick Sibomana, Maybin Kalengo, Lamine Moro, Mustapha Seleman na Sadney Urikhob ‘Aguero’

JK AFUNIKA
Wakati mgeni rasmi katika hafla hiyo akiwa ameshaingia na shughuli kuanza huku Mwenyekiti wa Kamati ya Hamasa, Anthony Mavunde akihutubia ghafla aliwasili mgeni maalumu Rais Mstaafu Jakaya Kikwete. Shangwe kubwa lililipuka wakati Kikwete akiwasili ikiwa ni mara yake ya kwanza kujitokeza katika shughuli za Yanga tangu na baada ya kutoka madarakani.
Baada ya Mavunde kumaliza hotuba yake iliyokuwa na sura ya kuifanya Yanga iwe klabu bora kiuchumi kwa kupendekeza njia za kutafuta mifumo bora ya uendeshaji, ilitimu wakati wa Kikwete kuzungumza.
Katika salamu zake Kikwete alimpongeza Waziri Majaliwa kwa kufika kwake katika hafla ya Yanga kwa kuwa huo ndiyo uongozi.
Kikwete alisema ukiwa kiongozi unatakiwa uwatumikie watu wote.
“Ukishakuwa kiongozi hutakiwi kubagua unatakiwa uwatumikie wote bila upendeleo wa kile unachokipenda, hivyo kufika kwako hapa nakupongeza sana ingawa sijui ni timu gani unashabikia,” alisema Kikwete huku akishangiliwa kwa nguvu karibu ukumbi mzima.

AFICHUA MAZITO
Akiendelea na hotuba yake Kikwete alifichua siri mbili, kubwa moja ni ile ya kuisaidia Simba fedha Sh30 milioni zilizosaidia kununuliwa eneo la Bunju ambalo wekundu hao wanataka kujenga uwanja.
“Jambo la pili ni hivi nilivyokuwa Rais alikuja Rage (Ismail aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba) akaniambia wamepata eneo kule Mabwepande sasa wanashida na Sh30 milioni ili wakalipie nikamwambia hakuna shida nikawapa,” alisema Kikwete.
Hata hivyo Kikwete aliwataka mashabiki wa Yanga kubadilika na kurudi viwanjani kuishangilia timu yao huku pia akiutaka uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha inawekeza katika soka la vijana na kuacha kutegemea wachezaji wa kutoka nje ambao hawaisadii timu ya taifa.

MAJALIWA ATAKA YANGA IMARA
Mgeni rasmi Majaliwa katika salamu zake aliipongeza Yanga kwa kuwa licha ya kucheza ligi msimu uliomalizika lakini walipambana vikali na kushika nafasi ya pili na kwamba hawakubebwa.
“Yanga ilikuwa na hali mbaya, lakini ilipambana yenyewe na kushika nafasi ya pili niwapongeze sana na niseme Yanga haikubebwa ilipambana,” alisema Majaliwa. Aidha Majaliwa alimpongeza Kocha Mwinyi Zahera akisema kocha huyo ni kocha mzuri ambaye alioisaidia klabu hiyo.
“Mimi kitaaluma ni kocha pia ni mkufunzi niseme Zahera ni kocha mzuri aliyeisaidia sana Yanga, mwisho niseme hakuna Ligi bora bila Yanga imara na hakuna simba imara bila Yanga imara.”

YAVUNA SH920  MIL
Wakati Majaliwa akimaliza hotuba yake akichangia Sh10 milioni taslimu pia aliwasilisha salamu za mfanyabiashara Rostam Aziz ambaye ni shabiki wa Yanga aliyeahidi Sh200 milioni atakazowasilisha akirejea kutoka safarini Marekani na kuufanya ukumbi kulipuka kwa shangwe. Naye Mavunde alitoa salamu kutoka Kampuni ya GSM ambayo iliahidi kutoa Sh300 milioni na shangwe kubwa kulipuka.
Naye Kikwete aliahidi kutoa Sh5 milioni katika kutunisha mfuko huo na mwishoni kamati hiyo ilianika fedha zote zilizokusanywa ikielezwa kuwa michango na ahadi jumla ni kiasi cha Sh920 milioni.

MAKONDA ATOA UWANJA
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema ameguswa na jinsi Rais Mstaafu Kikwete alivyoisaidia Simba na ameamua kuipa Yanga eneo la kujenga uwanja eneo la Kigamboni.
“Nimeguswa sana na jinsi Rais Mstaafu Kikwete alivyoisaidia Simba nami niseme kwa niaba ya serikali nimeamua kuipa Yanga eneo la kujenga uwanja Kigamboni na Jumatatu nitakuwa na watu wa ardhi na Yanga waje wapokee, ninachotaka kuona wakati Simba ikitokea Bunju Yanga itokee kigamboni na wakutane Uwanja wa Mkapa,” alisema Makonda huku akishangiliwa kwa nguvu na kabla ya Makonda kumaliza kwa staili hiyo, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Iramba Magharibi aliahidi kuichangia Yanga mchezaji mmoja mzawa kwenye usajili wa msimu ujao.

KILOMONI AIBUKA
Wakati wageni wazito wakitoka ukumbini ghafla aliibuka mmoja wa Wazee wa Baraza la Wadhamini wa Simba, Hamis kilomoni na kuharibu utulivu kutokana na kushangiliwa kwa nguvu.
Kilomoni alisikika akisema amealikwa na Yanga na hakuona shida ya kutofika ukumbini hapo kwani kuibuka kwake hakuna maana amefukuzwa Simba.