Pazi ampa mchongo Dida wa kumng’oa Manula

Muktasari:

Kakolanya amejiunga na Simba baada ya kushindwana na Yanga tangu msimu uliokwisha hivyo kushindwa kucheza mechi kadhaa za mzunguko wa pili.

Dar es Salaam.Kipa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Iddi Pazi amesema kipa Deogratius Munishi (Dida) anawezo wa kumtoa katika reli, Aishi Manula katika kikosi cha Taifa Stars.

Pazi aliyetamba Simba na Stars, alisema, kipa huyo anayemaliza mkataba na Simba aende kutafuta maisha mengine ya soka nje ya Tanzania.

"Dida alipaswa kuwa kwenye kikosi cha Afcon, tatizo Simba hawakumpa nafasi ya kuonekana," alisema Iddi Pazi na kuendelea.

"Ili amchalenji Manula, kipa huyo hana budi kutafuta timu ambayo itampa nafasi ya kucheza muda wote nje ya Tanzania.

"Kama ataamua kubaki hapa nchini pia aende kwenye timu itakayompa nafasi ya kucheza muda wote, akifanikiwa katika hilo hakosi namba timu ya Taifa," alisema.

Alisema kati ya makipa bora ambao yeye anawaamini miongoni mwao ni Dida, lakini ameonekana hafai kwa kuwa hapati nafasi ya kucheza.

"Ni ngumu sana kwenye timu unapomkuta kipa namba moja halafu akuachie nafasi ya kucheza, nasema hivyo kwa kuwa imewahi kunitokea mimi na nikapoteza namba kabisa," alisema Pazi.

Akizungumzia nafasi ya Beno Kakolanya aliyesaini mkataba wa miaka miwili Simba, Iddi Pazi alisema bado atakuwa na changamoto ya namba.

"Beno alishajenga jina tangu akiwa Yanga, hivyo alipaswa kuangalia timu ambayo itampa nafasi ya kucheza, pale Simba sijui, wacha tusubiri tuone kwani tayari amemkuta Manula ameshaweka mizizi na ndiye kipa tegemeo," alisema Pazi.