Mbona iko hivi: Usishangae kuna wachezaji wa mashabiki na wachezaji wa makocha

Muktasari:

Huenda fursa hii isijirudie tena kwangu. Huenda huu ndiyo wakati pekee ambao nitaweza kuandika wakati Taifa Stars iko mashindanoni. Huu ndiyo ukweli mchungu kuhusu mchezo wa soka na Tanzania yetu.

MARA ya kwanza, na ya mwisho kwa Tanzania kushiriki katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 1980, sikuwa nimetimiza hata mwaka mmoja duniani.
Kwa sababu hiyo, katika muda huu wote ambao timu yetu itakuwa Misri, nitautumia kuandika mambo yanayoihusu timu na mashindano hayo pekee.
Huenda fursa hii isijirudie tena kwangu. Huenda huu ndiyo wakati pekee ambao nitaweza kuandika wakati Taifa Stars iko mashindanoni. Huu ndiyo ukweli mchungu kuhusu mchezo wa soka na Tanzania yetu.

Mkude na Ajib
Nina bahati kwamba wachezaji hawa wawili; Jonas Mkude Gerald na Ibrahim Ajibu, nilifanikiwa kuanza kuwaona wangali vijana wadogo kabisa.
Wote walikuwa wachezaji wa timu ya vijana ya Simba iliyokuwa chini ya Selemani Matola na Amri Said. Walikuwa wachezaji wawili wazuri na viongozi wote wa Simba walikuwa na matarajio makubwa nao.
Hata hivyo, baada ya Emmanuel Amunike –Kocha Mkuu wa Taifa Stars, kutangaza kuwaacha katika kikosi chake kilichokwenda Misri, mengi yamezungumzwa kuwahusu. Hili jambo limewagawanya wadau wa soka karibu nusu kwa nusu.
Niseme jambo moja ambalo sote tunakubaliana; kwamba Ajibu na Mkude ni wachezaji wazuri. Uzoefu wangu kwa soka la Tanzania na wachezaji wetu unaonyesha kwamba, si jambo rahisi kudumu katika vilabu vikubwa vya Simba na Yanga kwa takribani misimu mitano. Ni lazima uwe mchezaji mzuri na mwenye sifa za ziada.
Zaidi ya Mkude na Ajibu, Simba ile ya vijana ilikuwa pia na wachezaji kama Abdallah Omar Seseme, Hassan Isihaka, Hassan Khatib, Miraji Athumani Madenge, Haruna Chanongo, Ramadhani Kipalamoto na Edward Christopher Shija. Kati ya wote hao, ambaye angalau alipata nafasi ya kwenda Misri na Miraji tu, lakini yeye sasa ni mchezaji wa Lipuli ya Iringa.
Wengine wote sasa wanachezea katika klabu nyingine, lakini Mkude na Ajibu bado wanacheza katika vikosi vya kwanza vya Simba na Yanga. Tusipoteze muda hapa kusema wachezaji hawa viwango vyao havitoshi.  Kuna sababu za nje ya uwezo wa uwanjani na hili ndilo eneo ambalo ningetaka kuliangalia leo.

Wachezaji wa
Makocha
Makocha wote duniani huzungumzia au hufurahia kuwa na wachezaji ambao hupenda kuwaita wachezaji wa timu. Hawa ni wachezaji ambao namna pekee ya kuwafahamu ni lazima uwe karibu sana na timu.
Kocha maarufu zaidi duniani kwa sasa, Jose Mourinho, alizungumza na Kituo cha Televisheni cha RT cha Russia mwanzoni mwa mwezi huu na alisema wachezaji ambao, aliwapenda na alikuwa karibu nao zaidi ni wale ambao pengine wala hakuwa akiwapanga mara kwa mara kwenye timu zao.
Hawa ni wale wachezaji ambao walikuwa hawanuni mazoezini wala hawalalamiki kama hawapangwi. Wanacheka, wanasapoti wenzao na wanaelewa kwanini kocha kaamua alivyoamua.
Wakati nikiwa kiongozi wa klabu ya Simba, mchezaji mmoja alikuwa akinifurahisha kuliko wengine wakati ule kwa sababu ya tabia zake. Alikuwa akiitwa Raymond Dotto.
Ray hakuwa akipangwa kama kina Miraji, Ajibu na Mkude. Mara nyingi alikuwa akianzia benchi. Lakini Ray alikuwa wa kwanza kuimbisha nyimbo wenzake, kuwahi mazoezini na wakati mwingine hata kusaidia kupanga ‘koni’ za mazoezi uwanjani.
Na kama mishahara kwa wachezaji imechelewa, Ray hakuwa wa kwanza kulalamika. Na rafiki zake walikuwa wachezaji waliokuwa wakianza kila mechi. Sasa huyu ndiyo mchezaji wa makocha.
Kama kocha anakwenda kwenye mashindano yoyote ambayo atahitaji kukaa na wachezaji kwa zaidi ya wiki moja au mbili, atahitaji kuwa na wachezaji wazuri kwa kadiri itakavyowezekana lakini pia atahitaji kuwa na wachezaji ambao, wataifanya kambi kuwa tulivu na yenye hamasa.
Ikumbukwe pia wachezaji ambao watacheza idadi yao mara nyingi huwa haizidi 16 au 17 na maana yake, wachezaji watano au sita wanaweza kuchaguliwa kwenye kikosi na wasicheze hata mechi moja katika mashindano yote. Katika hawa wasiocheza kabisa, unahitaji kuwa na wachezaji wa aina ya Ray.
Kuna upande mwingine tofauti wa wachezaji wa aina ya kina Raymond Dotto. Hawa ni wale ambao nimeona mfano wao katika wakati mfupi niliokaa kama kiongozi wa Simba.
Mfano huu ni wa hayati Patrick Mutesa Mafisango. Mzaliwa huyu wa DR Congo alikuwa mchezaji mzuri ndani ya uwanja, lakini alikuwa mzuri pia nje ya uwanja. Bahati mbaya ni kuwa mashabiki hawajui sana kuhusu mambo ya nje ya uwanja au mazoezini. Mashabiki wanajua tu kuhusu kinachofanyika viwanjani. Zaidi kwa mashabiki mchezaji mzuri ni yule anayefunga sana mabao ama kuokoa michomo mikali langoni.
Lakini, kwa kocha mchezaji mzuri anaweza kuwa nje ama ndani ya uwanja.
Wakati mmoja Simba ilikwenda Sudan kwenye mashindano ya kimataifa. Tulipofika kule, wenyeji walituwekea vyakula ambavyo wachezaji hawakuvipenda na morali ilishuka sana.
Ni Mafisango na Victor Costa ‘Nyumba’ ndiyo waliojitolea kupika ugali mkubwa kiasi cha kutosha wachezaji wote.
Ikatafutwa mboga na nakumbuka mpaka leo vichekesho ambavyo Mafisango alikuwa akitoa wakati akipika ugali.
Si tu kwamba Mafisango alikuwa akipika, lakini alikuwa mhamasishaji mkuu wa mazoezi wakati timu ikiwa mazoezini.
Simba ilipokwenda Algeria kucheza na Setif na wenyewe kufunga geti wakati baridi ikiwa kali ili Simba iathirike, ni marehemu Mafisango aliyewahamasisha wenzake waanze mazoezi palepale nje ya uwanja ili wasipigwe na baridi.
Huyu sasa alikuwa mchezaji ambaye kocha na watu wa benchi la ufundi wanatamani wawe naye wakati wanakwenda vitani.
Inawezekana hana uwezo mkubwa ndani ya uwanja, lakini umuhimu wake uko kwenye timu kuliko kwa mashabiki. Mafisango alikuwa na bahati kwa kuwa alikuwa mchezaji mzuri pia, lakini hata kama angekuwa ana uwezo wa kawaida, kwa tabia za namna hii, makocha wangempenda tu.
Tofauti na sisi mashabiki, makocha wana mawazo yao na wana hisia zao pia. Kwa bahati mbaya, mashabiki wengi hawaoni vitu vya nje ya uwanja ambavyo makocha wanaviona kwa sababu wanaishi na wachezaji kila siku.
Amunike amecheza AFCON akiwa na Nigeria. Amecheza Barcelona na anajua nini hasa anahitaji kwa wachezaji wake.
Anajua nini anahitaji kwa wale 11 au 14 ambao watacheza mechi zote na nini anahitaji kwa wale ambao, atasafiri nao na pengine hawatacheza hata mechi moja.
Anajua wapi ni wachezaji wa mashabiki wanaomsaidia kwenye matokeo mazuri na anajua wepi ni wachezaji ambao, atakaa nao mashindanoni na watafanya awe na kambi nzuri.