Kibabage: Msuva amenipa siri zote za Diffa El Jadida

Muktasari:

Kibabage atakuwa mchezaji wa pili wa Kitanzania baada Saimon Msuva kujiunga na Difaa El Jadida inayoshiriki Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’.

Dar es Salaam. Chipukizi wa Mtibwa Sugar, Nickson Kibabage amejiunga na Difaa El Jadida ya Morocco kwa mkataba wa miaka minne.

Kibabage amefichua kuwa baada ya kupata dili la kujiunga timu hiyo, alifanya fasta mawasiliano na Saimon Msuva ili kujua maisha ndani ya klabu hiyo yalivyo.

Beki huyo wa timu ya taifa chini ya umri wa miaka 20, alisema Msuva alimweleza kuwa Morocco ni sehemu sahihi ambayo itamfanya soka lake likue kwa kiwango kikubwa.

“Saikolojia yangu nimeiandaa kukabiliana na changamoto ya Lugha, sidhani kama naweza kushindwa kuendana na program zao hata kama kiarabu sikielewi, bahati nzuri ninaongea na kuelewa Kiingereza.

“Siku zote nilikuwa nikitamani kupata nafasi ya kucheza mpira nje ya nchi na ninamshukuru Mungu jambo hilo linaenda kufanikiwa kwa sababu tayari nimeshakuwa mchezaji wa Difaa,” alisema Kibabage.

Kibabage ni beki wa kushoto, alikuwa miongoni mwa wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ ya mwaka 2017, iliyoshiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana chini Gabon.