Staa amshangaa Ajibu, Mogella apigilia msumari

Muktasari:

Alimuelezea Ajibu kwamba kwa kipaji alichonacho angekuwa kwenye anga za mastaa wa Ulaya, akimlinganisha na mchezaji wa zamani wa Real Madrid, Zinedine Zidane aliyedai alikuwa na kipaji kikubwa na cha kuvutia ambacho alikitendea haki inayomfanya aheshimike mpaka leo

STAA wa soka la wanawake nchini, Mwanahamisi Omary ameamua kumfungukia Ibrahim Ajibu kwa kumpa ujumbe mzito kuhusu maisha yake ya soka kwamba nafasi anayoipata kwa sasa ajaribu kuitazama kwa faida ya maisha yake ya baadaye.
Mwanahamisi ambaye anakipiga Simba Queens na Twiga Stars, alianza kwa kusema kuwa kuna funzo kwa wachezaji wenye majina makubwa mbele ya jamii kutambua ipo siku ustaa utabakia pembeni na kubaki na uhalisia wao au majina ya wazazi wao.
Alimuelezea Ajibu kwamba kwa kipaji alichonacho angekuwa kwenye anga za mastaa wa Ulaya, akimlinganisha na mchezaji wa zamani wa Real Madrid, Zinedine Zidane aliyedai alikuwa na kipaji kikubwa na cha kuvutia ambacho alikitendea haki inayomfanya aheshimike mpaka leo.
Alishangazwa kuona Ajibu amekuwa mchezaji ambaye anapiga ruti na timu za nyumbani, akijiuliza anakwama wapi kuona fursa ya kucheza nje kama alivyo Mtanzania mwenzake Mbwana Samatta, anayekipiga Genk ya Ubeligiji na sasa anahusishwa na timu mbalimbali za Ulaya.
“Huwa najiuliza maswali mengi juu ya Ajibu, huenda wapo wadau wa soka Tanzania wanaojiuliza kama mimi, staa huyo anakwama wapi mpaka kushindwa kwenda nje? Unaona anapiga ruti mara Yanga kesho Simba, anashauriwaje na watu wake wa karibu kuona kipaji chake kinatakiwa kutikisa Ulaya ili taifa lipate sifa kupitia yeye kama ilivyo kwa Mbwana Samatta?” alihoji.
“Ajibu kaka yangu anapaswa kujitambua na kujua kwamba umri unakwenda na ustaa alionao leo kesho hautakuwepo watakuja wengine kwenye zamu zao, atabakia na jina halisi alilopewa na wazazi wake, sina nia ya kumsema ama kumsimanga la, huyo ni aikoni ya wengi mimi ni mmojawapo.
“Apambanue hilo mapema ili soka lake likiisha ajiwekee heshima kama ilivyo kwa wazee wetu kina Zamoyoni Mogella, kocha Abdallah Kibadeni, Boniface Mkwassa na wengine wengi, hilo naliona kwa Samatta anajijengea misingi ya kuheshimika kwa baadaye.”
Staa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella aliamua kupigilia msumari kabisa kwa kudai wachezaji wakionja raha za klabu kongwe, basi ni vigumu kwao kuona thamani ya vipaji vyao ambavyo vinaweza kuvuna mamilioni ya pesa kuliko wanazopata nchini.
“Siku zote huwa nasema Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu hawakuathiriwa na virusi vya Simba na Yanga, ila wengine hao hata ungewaambia neno gani ngumu kufumbua macho na kuona fursa ambazo zipo mbele yao na zinawasubiri wao kuamua,” alisema.
“Sio Ajibu peke yake ndiye anaonekana anashindwa kwenda kucheza nje, wapo wachezaji wengi wasiojua thamani yao, mpaka mwingine unaishia kuwashangaa ingekuwa fursa hizo zipo kipindi tunacheza basi tungetikisa sana Ulaya.”