Mike Tyson amkalisha chini Jean Claude Van Damme

Muktasari:

Kwa sasa Tyson ni kama kazaliwa upya. Si tena yule mtu mbaya. Umri umembadilisha, mitihani ya kufilisika imemfundisha. Mke wake, Kiki amemfanya awe mwanaume bora.

Dar es Salaam. KATIKA sehemu iliyopita ya makala haya ya bingwa wa dunia wa zamani wa ndondi za uzito wa juu, Mike ‘Iron’ Tyson, tuliona alivyookolewa na mrembo katika utumiaji wa dawa za kulevya na mipango ya kutaka kujiua na jinsi alivyoanza kukamata upya mkwanja. Pata sehemu hii ya mwisho ya simulizi la mkali huyo asiyesahaulika kwenye ngumi...
***
HIYO one-man show akaichukua na kuifanya ziara ya majiji 36. Akaiita Mike Tyson: Undisputed Truth. Tyson akawa anazunguka kusimulia maisha yake ya ndondi jukwaani. Mapene yakasoma benki. Mtandao wa Televisheni wa HBO waliichukua shoo hiyo ya Tyson na kuirusha hewani Novemba 13, 2013. Hela hizo zikaongezeka.
Oktoba 2012, Tyson alianzisha taasisi ya kukuza na kusimamia watoto wenye vipaji vya ndondi hasa wanaotoka kwenye ya maisha hohehahe. Taasisi hiyo inaitwa “Mike Tyson Cares Foundation”. Akaanzisha bonge la gym ambalo hutumika kukuza watoto na kurekodi vipindi vyake vya televisheni.
Kampuni ya kupromoti ndondi ya Acquinity Sports ikaona fursa kupitia Tyson. Wakampa hisa Tyson, kisha wakabadili jina la kampuni yao kuwa Iron Mike Production.
Televisheni ya Fox Sports 1 ikaona dili. Ikafanya ‘series’ za dokumentari ya maisha binafsi ya Tyson, wakaiita Being Mike Tyson (kuwa Mike Tyson). Salio benki likazungumza.
Novemba 2013, Tyson alitoa kitabu chake cha kwanza chenye jina “Undisputed Truth”. Kilitisha kwa mauzo na kuingia kwenye chati za mauzo ya The New York Times Best Seller.
Mamilioni ya Dola yaliingia kwa fujo kwenye akaunti ya Mike.
Series za katuni ya “Mike Tyson Mysteries”, inayomwonesha Tyson katika uhusika wa kufumbua mafumbo mbalimbali magumu, huku pia sauti yake ikisikika ni mradi mwingine ambao unamjaza Tyson dola nyingi ambazo Wamarekani huziita Benjamins.
Wimbo wa Madonna ‘Iconic’, uliopo kwenye albamu ya ‘Rubel Heart’, utamsikia Tyson anaongea mistari kadhaa mwanzoni kabisa. Hapohapo Tyson yupo kwenye muvi ‘Ip Man 3’ pamoja na mtu mbaya Donnie Yen. Pesa zinampenda Mike.
Tyson pia ana YouTube Channel kwa kushirikiana na kampuni ya Shots Studio. Huzalisha komedi na vipande vya video za Tyson. Hiyo yote ni kuhakikisha fedha zinajaa.
Mei 2017, Tyson alitoa kitabu alichokiita ‘Iron Ambition’ ambacho kimejaa maelezo kuhusu namna alivyoanza ndondi na kocha wake wa kwanza, Cus D’Amanto. Mahela mengine hayo yanaingia.
Tyson ni balozi wa magari ya Australia, Ultra Tune.
Ubalozi ameupokea kutoka kwa staa wa Hollywood, Jean-Claude van Damme. Aisee, pesa zinazidi tu kumiminika. Tofauti na zamani alikuwa anapata pesa nyingi na zikawa hazitoshi kwa sababu ya matumizi makubwa, sasa hivi anatumia kwa nidhamu na fedha ni nyingi sana benki.
Anahudumia familia yake vyema. Watoto wake sita waliobaki wana furaha kumwona baba yao ni baba mwajibikaji kwa familia. Mtoto mmoja wa Tyson alifariki dunia Mei 2009.
Hana maisha ya wapambe na msururu wa watumishi. Ana wafanyakazi wachache.
Si teja tena. Starehe anafanya kwa kiasi. Muda mwingi yupo bize na kazi kutengeneza fedha ili familia yake ipate mahitaji muhimu na watoto wapate urithi wao. Kwa sasa Tyson ni kama kazaliwa upya. Si tena yule mtu mbaya. Umri umembadilisha, mitihani ya kufilisika imemfundisha. Mke wake, Kiki amemfanya awe mwanaume bora.
Kwa sasa anaminya kwenye mjengo wake wa kifahari uliopo Henderson, Nevada ambao aliununua Desemba 2016 kwa fedha dola 2.5 milioni (Sh5.8 bilioni). Magari yake yote yanatembea. Mafuta na gesi sio tatizo kwake. Tyson anasema, shukrani zake nyingi ni kwa mkewe, Kiki. Anasema alikuwa mshamba sana wa fedha ndiyo maana ziliisha.
Hata hivyo, anasema yeye ni mwenye bahati sana kumpata Kiki. Maana alimrudisha kwenye reli. Anakiri pia kuna marafiki wachache walimsaidia asizidi kupotea.