Coutinho anashangaa watu Barcelona hawamtaki

Tuesday June 11 2019

 

BARCELONA, HISPANIA. PHILIPPE Coutinho anataka kuachana na Barcelona katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi. Hilo ndilo lisemwalo.
Lakini shida inakuja ni kwamba anashangaa hakuna hata timu moja ambayo ipo siriazi kwenye kuinasa saini yake zaidi ya kusikia tu huko kwenye magazeti.
Ripoti za kutoka Hispania zinadai Coutinho anashangaa kuona hakuna ofa yoyote rasmi iliyoletwa huko Nou Camp kwa ajili ya kuhitaji huduma yake katika kipindi hiki cha uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya baada ya hapo awali jina lake kuhusishwa na Manchester United na Chelsea.
Mundo Deportivo linaripoti Coutinho anajiona kama ameishiwa baada ya kutopata ofa yoyote rasmi wakati inafahamika wazi klabu yake ya Barcelona imefungua milango ya kumpiga bei Mbrazili huyo ili inase mchezaji mwingine baada ya kuona ameshindwa kufanya vyema kwenye kikosi hicho.
Kocha wa Barcelona, Ernesto Valverde, amefichua hajapokea simu yoyote inayoulizia kupatikana kwa huduma ya Mbrazili huyo hasa katika kutambua ada yake anayouzwa na mshahara atakaotaka kulipwa.
Coutinho alitua Barcelona Januari mwaka jana kwa ada ya Pauni 142 milioni, ambayo inashikilia rekodi kwenye kikosi hicho cha Nou Camp hadi sasa. Wababe hao wa La Liga kwa sasa wanapiga hesabu za kumsajili Antoine Griezmann.

Advertisement