Kesi Malinzi: Kigogo TBL aeleza alivyobaini ubadhirifu TFF

Muktasari:

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wanaendelea kusota rumande kwa sababu wanakabiliwa na mashitaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Richard Magongo ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu walivyogundua upungufu baada ya kufanya ukaguzi ndani ya Shirikisho la Soka Tanzani (TFF).

Magongo ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Benki ya Barclays alieleza hayo jana wakati akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Maira Kasonde katika kesi inayomkabili aliyekuwa raisi wa TFF Jamal Malinzi na wenzake.

Akiongozwa na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Leonard Swai, shahidi huyo alidai Mei 2012 kampuni ya TBL iliingia mkataba na TFF kudhamini timu ya soka kwa miaka mitano.

Alidai kila mwaka kampuni hiyo ilikuwa ikitoa Dola2 milioni na zilikuwa zikitolewa kila baada ya robo mwaka kwa kipindi cha miaka mitano TBL ilitoa Dola10 milioni.

Magongo alidai katika masharti ya TBL ilitaka TFF kuleta hesabu ya kila robo mwaka kabla ya kupewa fedha nyingine.

"Katika kupewa mkopo TBL waliitaji nyaraka za kuthibitisha matumizi, zilitakiwa kufuatwa na TBL na kamati nyingine ya usimamizi na ukaguzi wa matumizi kabla ya kuwapa fedha nyingine,”alidai shahidi huyo.

Shahidi huyo alieleza walianza kukagua mwaka 2013, walifanya ukaguzi robo ya mwisho ya mwaka 2017.

Shahidi huyo alidai baada ya kupitia ripoti waligundua kasoro ambapo fedha za wadhamini zilizotumika hazikuwa na nyaraka za kutosha kuthibitisha uhalali wa matumizi.

"Hakuna mkataba wa ukopeshaji kati ya Malinzi na TFF au nyaraka zozote zikionyesha Jamali Malinzi kuweka fedha kwenye akaunti za TFF au risiti za matumizi.

Shahidi huyo alidai Mei 8, 2014 katika orodha ya matumizi ambayo hayakuwa na nyaraka ni Dola 902,981.98 Hakimu Maira aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili Juni 20 mwaka huu itakapoendelea na usikilizwaji.

Mbali na Malinzi washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa TFF,  Nsiande  Mwanga, Meneja wa Ofisi TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja  wanakabiliwa na mashitaka 30 katika  kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017.

Mashitakiwa hayo yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa dola za Marekani 173,335.

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wanaendelea kusota rumande kwa sababu wanakabiliwa na mashitaka ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.