Polisi yakabidhi mwili wa Mwangata kwa familia

Muktasari:

Enzi za uhai wake, Mwangata alishinda medali ya fedha ya michezo ya Afrika, ameiwakilisha nchi kwenye Olimpiki na michezo ya Jumuiya ya Madola kabla ya kustaafu na kuwa kocha wa klabu ya ngumi ya JKT na timu ya Taifa.

Dar es Salaam. Familia ya aliyekuwa bondia na kocha wa timu ya Taifa ya ngumi za Ridhaa, Benjamin Mwangata imekabidhiwa mwili wa bondia huyo tayari kwa mazishi.

Mwangata aligundulika amefariki jana Asubuhi baada ya majirani kubomoa mlango na kumkuta nyumbani kwake akiwa amefariki.

Baada ya kifo hicho, polisi waliiuchukua mwili wake kwa uchunguzi zaidi ambapo Leo Jumatatu mchana wameukabidhi kwa familia kwa ajili ya kuendelea na taratibu za mazishi.

Mke wa marehemu, Ursula Mwangata alisema familia imekabidhiwa mwili huo mchana huu katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

Alisema baada ya kukabidhiwa mwili huo, familia itakutana kwa ajili ya kupanga taratibu za mazishi ya mwanamasumbwi huyo.

"Tumeambiwa na madaktari kuwa Mwangata alikosa msaada wa haraka, ilikuwa ni presha," alisema mke huyo wa marehemu kwa masikitiko.

Alisema Mwangata alirejea nyumbani Alhamisi baada ya kuondoka Jumatano na familia kwenda Kibaha kwa mmoja wa watoto wake kwa ajili ya kusherehekea sikukuu ya Eid, hivyo familia ikabaki kule akarudi peke yake.