JKT yarudi kileleni, Pazi yajinasua Ligi ya kikapu Dar

Monday June 10 2019

JKT, yarudi, kileleni, Pazi, yajinasua, Ligi kikapu, Dar es Salaam, Mwanaspoti

 

By Imani Makongoro

Dar es Salaam.Maafande wa Jeshi wa JKT wamebakiza mechi moja kuweka rekodi mpya ya kutofungwa kwenye Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA) huku vigogo Pazi wakijinasua kwenye 'danger zone'.

JKT imekalia usukani wa Ligi hiyo baada ya kuishusha Oilers jana Jumapili ndiyo timu pekee ambayo haijapoteza mechi huku mchezo wake wa jana Jioni ikichomoza na ushindi wa pointi 76-59 dhidi ya Pazi.

Timu hiyo ambayo inapambana kusaka ubingwa wa msimu huu ina pointi 28 ikiwa imeshinda michezo yote 14 na imesalia na mechi moja ili kuhitimisha ratiba ya mzunguko wa kwanza.

Vigogo wengine kwenye Ligi hiyo, Pazi imejinasua kutoka kwenye 'danger zone' licha ya kufungwa mechi yake, lakini matokeo ya Youngstars dhidi ya Tanzania Prison yaliibeba Pazi katika msimamo.

Pazi imecheza mechi 13 na kufungwa nane ambapo awali ilikuwa ni ya tatu kutoka mwisho, lakini sasa nafasi hiyo inashikiliwa na Youngstars ambayo imecheza mechi 14 na kufungwa 11.

Youngstars ilikubali kipigo cha pinti 75-57 dhidi ya maadfande wa Tanzania Prisons hivyo kushushwa hadi nafasi ya tatu kutoka mwisho mbele ya Jogoo ambayo ni ya pili kutoka mwisho ikiwa imefungwa mechi zote 15 na Segerea BC ni ya mwisho katika msimamo japo ina mchezo mmoja mkononi kuhitimisha mzunguko wa kwanza.

Advertisement

Bingwa Mtetezi Savio imeendelea kung'ang'ania nafasi ya nane kwenye msimamo kwa wiki tatu mfululizo ikiwa imeshinda michezo minane na kufungwa mechi sita mzunguko wa kwanza.

Msimu wa 2017, Savio ilitwaa ubingwa bila kufungwa huku msimu wa 2018 ilitwaa ubingwa ikiwa imefungwa mechi moja dhidi ya mahasimu wao, Oilers.

Kocha wa Savio, Evarist Mapunda alisema hana presha na mechi za Ligi, atatetea ubingwa wake kwenye mechi za mtoano.

"Kikubwa ni kuingia kwenye play off, huko ndiko tutajua nani bingwa," alisema kocha huyo ambaye ameiongoza Savio kutwaa ubingwa mara tatu mfululizo.

Mkurugenzi wa Ufundi wa ufundi wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD), Gosbert Boniface alisema timu nane zitakazofanya vizuri kwenye Ligi hiyo zitacheza play off kusaka bingwa wa 2019.

 

Advertisement