Zahera apewa mchongo kuisuka Yanga

Monday June 10 2019

Mwanaspoti, Michezo, Mwanasport, Zahera, mchongo, kuisuka, Yanga

 

By OLIPA ASSA

MASHABIKI wa Yanga wanamkubali sana Mwinyi Zahera ambaye uwepo wake unatajwa kuwapa tumbo joto watani wao wa Simba, hii ni kwa sababu ya uwezo wake wa kuwatengeneza wachezaji  kufanya mambo makubwa uwanjani.
Lakini sasa unaambiwa kocha huyo amepewa mchongo wa kijanja na kama ataamua kuufanyia kazi ni wazi atazidi kufunika hasa kipindi hiki Yanga ikienda kukinukisha kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika sambamba na Simba.
Straika wa zamani wa Yanga anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao mengi katika msimu mmoja, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ amemuuma sikio Mkongomani akimweleza kuwa iwapo atamtumia Mwenyekiti wao, Dk Mshindo Msolla atatisha ile mbaya.
Mmachinga alisema Dk Msolla ambaye ana taaluma ya ukocha  uwepo wake Yanga ni kitu kikubwa endapo Zahera ataamua kumtumia kwa umakini.
Alisema Msolla ameingia Yanga kama mwenyekiti wa klabu na si kocha, lakini anaona kuna fursa nyingi za kufaidi madini yake kama benchi la ufundi litaamua kushirikiana naye kwenye masuala ya usajili.
Yanga inaendelea kusajili kwa ajili ya kuimarisha kikosi chao, jambo ambalo Mmachinga alimshauri Zahera akiona anahitaji zaidi undani wa wachezaji wazawa, basi anaweza kumshirikisha Dk Msolla ili kuweza kupata majembe ya maana.
“Msolla ni mwenyekiti anayefuata na kuzingatia kanuni na alishasema kwamba ameingia Yanga kwa ajili ya nafasi hiyo, lakini pia aliacha milango wazi ya ushauri kwa benchi la ufundi.
“Ndio maana namshauri Zahera akiona kama kuna umuhimu wa jambo hilo (la usajili) amshirikishe pia asiwe anakataa ushauri ingawa yeye ndiye anayetakiwa kusimamia kila kitu kwenye usajili,”alisema nyota huyo.  
Mmachinga anayeshikilia rekodi ya mabao 26 katika msimu wa 1999, alisema Yanga wamepata nafasi ambayo walikuwa wanaipigania ya kushiriki michuano ya kimataifa, jambo alilodai wanahitaji kupata kikosi imara.
“Lazima Yanga isajili wachezaji wenye viwango vya juu, mfano nafasi ya ushambuliaji ni muhimu sana kuangaliwa alikuwa Heritier Makambo akiumia huyo basi roho zetu zilikuwa juu, hivyo msimu ujao lazima wawe makini zaidi kuwa na watu wa kazi, ingawa nawapongeza wachezaji wote walifanya kazi kubwa mbele ya ukata.”

Advertisement