Bigirimana wa Yanga amtikisa Aussems, Ajibu abadili gia angani

Muktasari:

Bigirimana alisema wala hahofii ubora wa Simba na kwamba amekuwa na bahati kubwa ya kufanya vizuri katika mechi za watani wa jadi na anafahamu sasa hilo anatakiwa kulifanya dhidi ya wekundu hao.

KAMA anachokisema ndicho anachomaanisha ni wazi Wekundu wa Msimbazi lazima wajipange, kwani straika mpya wa Yanga, Issa Bigirimana amedai kutua kwake Jangwani sio kwa ajili ya kuuza sura, ila kupiga kazi na hata kama Yanga itampa mechi ya watani freshi tu.
Straika huyo amesema kama kuna mechi ambazo ana bahati nazo kwa kutupia kambani basi ni zile za ‘derby’ na kusema hata hao Simba ambao amesikia kwa misimu mitatu hawajawahi kuonja kipigo cha Yanga, basi wajiandae kwa sababu amekuja Tanzania kikazi.
Mbali na kufichua hilo, lakini akafunguka nafasi ambayo Kocha Mwinyi Zahera atampa mashabiki wa timu hiyo watafurahi kwa sababu anajua kufanya mambo.
Akizungumza na Mwanaspoti kutoka Rwanda anakomalizia mkataba wake ma APR, Bigirimana alisema wala hahofii ubora wa Simba na kwamba amekuwa na bahati kubwa ya kufanya vizuri katika mechi za watani wa jadi na anafahamu sasa hilo anatakiwa kulifanya dhidi ya wekundu hao.
“Naijua Simba ni timu kubwa, lakini jambo ambalo Simba na timu zingine kubwa zinatakiwa kutambua ni kwamba nimekuwa na bahati kubwa sana kufunga mabao muhimu katika mechi kubwa hasa za wapinzani wa jadi,” alisema.
Bigirimana akiwa na APR ya Rwanda mashabiki wa wapinzani wao, Rayon wamekuwa wakimwogopa na kumchukia kutokana na rekodi yake ya kuwafunga na hilo anataka kulihamishia Yanga.
“Ukiuliza hapa Rwanda watakuambia Rayon wamekuwa wakiona nipo uwanjani, tena nikicheza dhidi yao hawana raha kabisa, nimekuwa nafunga sana mechi kubwa hiyo, ndio sifa yangu kubwa hapa, hilo mtaamini nikianza kazi Yanga.”
Mshambuliaji huyo alisema anatambua Simba ina mabeki bora, lakini mashabiki wa Yanga wala wasiwe na wasiwasi kwa kuwa anaijua vyema kazi yake akiwa uwanjani.

NAMBA YA MAKAMBO Bigirimana alisema licha ya ubora wake wa kucheza nafasi nyingi kama winga wa kulia, lakini kama Yanga itakuwa na viungo wazuri wa kati basi kocha wake akimpa nafasi ya kucheza mshambuliaji wa kati atafunga sana.
“Mimi naweza kucheza nafasi nyingi pale mbele, lakini kama Yanga kutakuwa na viungo wazuri wa kati wakawa na ujuzi wa kutoa pasi za mabao, basi kocha akinipa nafasi ya kucheza kama namba tisa nitafunga sana.”

AJIBU ABADILI GIA
Katika hatua nyingine, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajibu amebadilisha gia angani kwa kufanya mzungumzo na mabosi wa Jangwani ili aongeze mkataba kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Ajibu ambaye mkataba wake umemalizika, amehusishwa kujiunga na watani wao wa jadi, Simba ambao wanasadikiwa kumsainisha mkataba wa awali.
Mchezaji huyo mwenye kipaji, hivi karibuni ilikuwa ajiunge na klabu maarufu barani Afrika, TP Mazembe ya DR Congo. Hata hivyo dili hili lilitoweka kutokana na sababu zisizo wazi.
Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti limezipata ni kwamba Ajibu alikutana na uongozi wa Yanga na kutoa masharti yake ambayo yakitimizwa, basi atasaini mkataba mpya. Mazungumzo na mchezaji huyo yalifanyika kwenye Hoteli ya White Sands wakati wa kambi ya timu ya Taifa, Taifa Stars na kwa sasa kaka yake anaendelea na mchakato huo.
Imeelezwa kuwa moja ya sababu za Ajibu na uongozi wa Yanga kuanzisha mazungumzo hayo ni hatua ya klabu hiyo kuingia katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa ambayo imemvutia.
“Kwa sasa mazungumzo yanaendelea na utakapofikia muda, suala la Ajibu litawekwa hadharani. Yanga haina matatizo na Ajibu, tofauti na suala hilo linavyochukuliwa,” kilisema chanzo  chetu ndani ya klabu hiyo.