Mike Tyson: Aokolewa na mrembo, awa mtamu upyaa

Muktasari:

Tyson alifunga ndoa na Kiki Juni 2009. Kuanzia hapo, kazi ya Kiki ikawa kumfumbua macho Tyson ili aache kulalamika giza, aone mwanga na ayaone maisha

KATIKA sehemu iliyopita ya makala haya ya bingwa wa dunia wa zamani wa ndondi za uzito wa juu, Mike ‘Iron’ Tyson, tuliona alivyogeuka teja baada ya kufilisika na kuanza kuwaza kujiua. Endelea…

TYSON AMEKUWA MTAMU
Sikia, nyakati za maumivu na kukata tamaa, unahitaji mtu wa kukushika mkono na kukupa moyo. Angalau mtu huyo akwambie kwa kukunong’oneza kuwa maisha hayajafika mwisho.
Tyson alihisi dunia imemwelemea. Pesa alishatumia zote zikaisha. Hakuwa na uwezo tena wa kupigana. Majukumu yalimwandama. Madeni nayo yakashika kasi.
Hapa Tyson alihitaji mtu wa kumpiga ngumi nyepesi kifuani upande wa kushoto palipo na moyo na kumwambia: “Come on bro, it’s not over yet. Huu siyo mwisho wa mchezo, nyanyuka upambane. Maisha bado yapo na dunia inakusubiri.”
Hii ni kwa yeyote, maisha yamegeuka juu chini. Unahisi mbele ni pagumu? Dunia imekuelemea na pengine walimwengu wanakucheka na kukuona kituko. Sikia, amka upambane. Kata rufaa. Maisha hayajafika mwisho.
Ubishi wako ndiyo rufaa. Inawezekana unahitaji imani tu ili maisha yawe mazuri. Nyakati zijazo neema zikishafunguka, utajiona mjinga ukikumbuka ulivyotaka kukata tamaa. Ulivyojaribu kujidanganya eti maisha yamefika mwisho.
Tyson ni mwenye bahati sana. Kipindi akiamini maisha yapo ukingoni, alitokea mwanamke, akamwambia “acha uoga wa maisha. Huu siyo mwisho.” Ooh, ni hapo Tyson alijikusanya na kurejea kwenye ulingo wa maisha kuendelea kupambana.
Ni kweli, katika ulingo wa ndondi Tyson alikuwa ameshapoteza uwezo wa kupambana. Ulingo wa masumbwi haumhitaji tena. Hata hivyo, ulingo wa maisha bado unamhitaji. Na pambano la maisha bado hajapoteza. Amini, kama bado unavuta pumzi, ujue pambano la maisha hujalipoteza. Amka pambana!
Mrembo Lakiha Spicer ‘Kiki’ alikuwa rafiki wa muda mrefu wa Tyson. Kipindi ambacho Tyson anaona mbele giza na maisha yapo ukingoni, Kiki alimwambia Tyson: “Giza la maisha unaloona ni kwa sababu umefumba macho. Fumbua macho utaona mwanga.”
Kipindi ambacho Tyson alioneka amefulia na asiyetamanika, Kiki alimuona ni mwanaume mzuri. Aliamini anahitaji kutulizwa na kila kitu kingekuwa sawa. Ona sasa, Tyson amekuwa mwenye furaha. Na maisha ni matamu.
Tyson alifunga ndoa na Kiki Juni 2009. Kuanzia hapo, kazi ya Kiki ikawa kumfumbua macho Tyson ili aache kulalamika giza, aone mwanga na ayaone maisha. Kweli, Tyson akaanza kuyaona maisha tena. Na anajishangaa kwa nini alikata tamaa kipindi kile.
Hatengenezi fedha za fujo kama kipindi kile alipokuwa bingwa wa dunia wa ndondi, nyakati akiudai ulingo wa masumbwi pesa nyingi ili apande kuchakaza watu kwa ndonga zake nzito, hata hivyo pesa anazipata na zinamfanya aishi maisha murua na familia yake.
Alipotuliza ubongo na kukubali kuwa mabilioni yake aliyoyapata kwenye ndondi yalishatoweka lakini maisha bado yapo, alianza kukusanya mikwanja kupitia milango mingine. Mwaka 2009 alicheza muvi yenye jina, “The Hangover”. Pesa zikaingia.
Mtu mzima akawa bize. Akaanza kurekodi documentaries mbalimbali na kuandika vitabu kuhusu maisha yake ya boxing, mafanikio na anguko lake. Akafanya one-man show kwenye jukwaa la Broadway Agosti 2012, akasimulia mishemishe zake za ndondi. Mpunga wa kutosha ukasoma benki.