Kamusoko, Kutinyu wala shavu AFCON

Muktasari:

Kamusoko ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na Yanga kumalizika wakati Kutinyu amejiunga na Horoya ya Guinea pia kama mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba wake na Azam FC.

Dar es Salaam. Ukiona cha nini jua kuna wenzio wanajiuliza watakipata lini.

Msemo huu ndio unaweza kuutumia kuelezea neema ambayo kiungo aliyetemwa na Yanga, Thaban Kamusoko ameipata baada ya kuteuliwa kwenye kundi la wachezaji 23 wa Zimbabwe watakaoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika nchini Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19

Baada ya kufanya vizuri kwenye hatua ya mwanzo ya maandalizi ya Zimbabwe kwenye iliyohusisha mechi za mashindano ya soka kwa nchi wanachama wa Baraza la Vyama vya soka Kusini mwa Afrika (COSAFA), Kamusoko ambaye ametemwa na Yanga, amepata fursa adhimu ya kushiriki mashindabno ya AFCON mwaka huu ambayo yatashirikisha nchi 24.

Mbali na Kamusoko, mchezaji mwingine ambaye amejumuishwa kwenye kikosi cha mwisho cha Zimbabwe ni aliyekuwa kiungo wa Azam FC, Tafadzwa Kutinyu hivi karibuni alikamilisha usajili wa kujiunga na Horoya ya Guinea

Kocha mkuu wa Zimbabwe, Sunday Chidzambwa ametangaza kikosi cha nyota wake 23 ambao wataitumikia timu hiyo kwenye AFCON ambapo kamusoko amejumuishwa kundini huku wachezaji tisa wakienguliwa kutoka kwenye kikosi cha awali kilichokuwa na wachezaji 34.

Katika hali ambayo haikutegemewa, jina la mshambuliaji Walter Musona wa Polokwane City halikujumuishwa na kocha Chidzambwa kama alivyofanya kwa beki wa Lusaka Dynamos, Dennis Dauda na mshambuliaji wa Leicester City, Admiral Muskwe

Kama ilivyotegemewa mastaa kama Khama Billiat wa Kaizer Chiefs, Kudakwashe Mahachi (Orlando Pirates), Knowledge Musona (Lokeren) na Marvelous Nakamba (Club Brugge) wamejumuishwa kwenye kundi hilo la wachezaji 23.

Kikosi hicho cha wachezaji 23 wa Zimbabwe watakaoshiriki AFCON kinawajumuisha makipa George Chigova (Polokwane City), Edmore Sibanda (Witbank Spurs) na Elvis Chipezeze (Baroka).

Mabeki walioitwa kikosini ni Jimmy Dzingai (Power Dynamos), Alec Mudimu (CEFN Druids), Teenage Hadebe (Kaizer Chiefs), Divine Lunga (Golden Arrows), Ronald Pfumbidzai (Bloemfontein Celtic) na Tendai Darikwa (Nottingham Forest).

Viungo, kocha Chidzambwa amewajumuisha Danny Phiri (Golden Arrows), Marshall Munetsi (Orlando Pirates), Marvelous Nakamba (Club Brugge), Tafadzwa Kutinyu (Horoya), Ovidy Karuru (AmaZulu), Khama Billiat (Kaizer Chiefs), Kudakwashe Mahachi (Orlando Pirates), Talent Chawapihwa (AmaZulu), Knowledge Musona (Lokeren) na Thabani Kamusoko (huru)

Washambuliaji walioitwa ni Nyasha Mushekwi (Dalian Yifang), Evans Rusike (SuperSport United),Tinotenda Kadewere (Le Havre) na Knox Mutizwa (Golden Arrows).