Harambee Stars kujipima ubavu kwa DR Congo

Muktasari:

Kabla ya kuchuana na DR Congo, Stars watashiriki katika mechi nyingine ya kujipima nguvu dhidi ya Madagascar Juni 7, mini Paris.

SHIRIKISHO la soka nchini FKF limeiratibia Harambee Stars mchuano wa kirafiki dhidi ya DR Congo ikiwa ni sehemu ya maandalizi yao ya kushiriki dimba la AFCON 2019 mwezi ujao.
Rais wa FKF, Nick Mwendwa kasema mechi hiyo itachezwa mjini Madrid, Uhispania Juni 15. Mchuano huo utakuwa mbadala wa mechi ya awali dhidi ya Gambia iliyokuwa imeratibiwa kuchezwa tarehe sawia mjini Paris, lakini ikafutiliwa mbali baada ya Mashirikisho ya mataifa husika kukosa kuafikiana.
Kabla ya kuchuana na DR Congo, Stars watashiriki katika mechi nyingine ya kujipima nguvu dhidi ya Madagascar Juni 7, mini Paris. Jumatatu ya wiki hii Kocha wa Stars, Mfaransa Sebastian Migne alianza maandalizi ya timu yake  akiingia kambini na wachezaji 16 kati ya 30 aliowaita.
Migne aidha aliweka wazi  ataendelea kukipanga pangua kikosi chake hadi kufikia Juni 15 na atachuja wachezaji saba watakaokuwa hawajamridhisha kabla ya kukabidhiana listi yake ya kikosi cha wachezaji 23 kwa waandalizi wa AFCON kwa mujibu wa sheria. Hatua yake hiyo anasema ni kuhakikisha anapata wachezaji wote bora anaoweza kuwanasa kuelekea kwenye kipute hicho.
“Wiki ijayo nitaipunguza kikosi hadi kubakia wachezaji 26 kisha 23 kwa kutegema nitakachokuwa nimekiona kwenye kambi hii” alisema.