De Ligt anaitaka Manchester United kinoma

Saturday May 25 2019
Lightpic

AMSTERDAM, UHOLANZI. NAHODHA wa Ajax, beki Matthis de Ligt amewaaminisha mashabiki kwamba anataka kwenda kujiunga na Manchester United baada ya kubonyeza kitufe cha like posti ya Rio Ferdinand kwenye Instagram iliyoonyesha Man United wakishangilia ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2008.
Man United wanatajwa kushika namba mbili kwenye mbio za kumsaka Mdachi huyo nyuma ya Barcelona ambao wanadaiwa kuwa na nafasi kubwa ya kupata huduma ya kinda huyo mwenye umri wa miaka 19.
Matthis de Ligt amewapa mashabiki wa Man United maneno kibao ya kuzungumza huko vijiwani wenzao kisa tu kitendo chake cha kuonyesha kupenda kile kilichopostiwa na Ferdinand kikionyesha mashujaa hao wa Old Trafford walipofanya yao huko Ulaya.
Shabiki mmoja aliandika: "Lindelof - De Ligt bonge ya kitu. Wow."
Lakini, kwenye posti hiyo ya Ferdinand kulikuwa na komenti nyingi tofauti, ambapo kuna shabiki mmoja aliandika: "Matthijs De Ligt anahitaji kupimwa akili kama anafikiria kujiunga na United."
Huku mwingine aliandika: "Kama De Ligt akisaini Manchester United nitatoa Dola 100 kwa kila mtu aliyetuma tena hii posti. Kila la heri."
Ishu ya De Ligt kuhama kwenye dirisha hili imekuwa na ugumu kidogo kutokana na wakala wake Mino Raiola kudaiwa kufungiwa kuzungumzia dili za kuhamisha mastaa wake. Man United waliwahi kuripotiwa kwamba wanaweza kufuta mpango wa kumsajili De Ligt kwa sababu ya historia ya baba yake kuwa mnene, kwamba huenda akaja kuwa kibonge huko mbele.

Advertisement