Makipa Petr Cech, Leno wampasua kichwa Emery

Muktasari:

Kipa Cech amecheza dakika 1,845 wakati Leno amecheza dakika 3,195. Cech amekumbana na mashuti 76 na kufungwa mabao 22, wakati Leno amekumbana na mashuti 158 na kufungwa mabao 45

London, England. UNAI Emery kichwa kinampasuka, yupo njia panda kuhusu kipa gani wa kumwaanzisha kwenye fainali ya Europa League kati ya Petr Cech na Bernd Leno.
Presha imekuwa kubwa kwa kocha huyo wa Kihispaniola na kukuna kichwa ampige chini Cech, ambaye atakuwa akicheza mechi yake ya mwisho kwenye kikosi hicho cha Arsenal au amweke benchi Leno.
Mashabiki wa Arsenal wanataka Cech awekwe benchi kwenye mechi hiyo dhidi ya timu yake ya zamani hasa baada ya kusikia  kipa huyo baada ya mechi hiyo anaweza kurudi Stamford Bridge kwenda kuwa bosi.
Staa wa zamani wa Arsenal, Tony Cascarino naye anaamini Leno ni chaguo bora kabisa la kipa kwenye fainali hiyo.
Cascarino alisema: "Petr Cech asichezee Arsenal kwenye fainali hiyo ya Europa League. Sio kwamba atakwenda kujiunga na Chelsea kama mkurugenzi wa michezo, ila ni kutokana na presha kubwa inayomkabili tofauti na Bernd Leno."
Lakini je, takwimu za makipa hao ndani ya uwanja kwa msimu huu zikoje? Kwa msimu huu, Cech amecheza mechi 21, wakati Leno amecheza mechi 36. Katika mechi hizo, Cech ameanzishwa zote, huku Leno akianza kwenye mechi 35. Kipa Cech amecheza dakika 1,845 wakati Leno amecheza dakika 3,195. Cech amekumbana na mashuti 76 na kufungwa mabao 22, wakati Leno amekumbana na mashuti 158 na kufungwa mabao 45. Makipa wote wamecheza mechi nane bila ya kuruhusu nyavu zao kuguswa huku Cech akiokoa hatari 55 na Leno akifanya hivyo mara 114. Eneo baya linalomkabili Leno ni kwamba amefanya makosa matano yaliyowafanya wapinzani kufunga, wakati Cech katika mechi zake alizocheza, hajafanya kosa lolote lililowapa bao wapinzani. Kazi ni kwake Emery.
Arsenal kwenye fainali hiyo ya Europa League itaikabili Chelsea huko mjini Baku.