Bocco, Kagere si wa mchezomchezo

Muktasari:

Kagere licha ya msimu wake wa kwanza katika Ligi, ameonyesha uwezo mkubwa kiasi cha kuwafanya mabosi wa Simba waanze kuumiza kichwa kwa namna ya kumbakiza msimu ujao.

Dar es Salaam. Hakuna ubishi kwamba washambuliaji John Bocco na Meddie Kagere ndio chachu ya ushindi wowote wa Simba baada ya wachezaji hao kuhusika katika mabao 39 yaliyofungwa na klabu hiyo katika Ligi Kuu.

Kagere amefunga mabao 23 huku Bocco akifunga 16 na kuwafanya kufikia idadi hiyo na kuwafanya kuwa washambuliaji hatari katika kikosi cha Simba.

Achana na ukali wao katika Ligi Kuu sasa, katika mchezo wao wa kirafiki waliocheza na Sevilla, Bocco na Kagere waligeuka kuwa mwiba baada ya wawili hao kucheza kwa maelewano ya hali ya juu.

Kasi ya Kagere na Bocco ilikuwa mwiba kwa mabeki Sevilla katika mchezo wa kirafiki uliochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Taifa, na Simba kufungwa mabao 5-4.

Katika mchezo huo Bocco alifunga magoli mawili dakika 8, 32, lakini muda wote alionekana kuisumbua safu ya ulinzi huku ushirikiano mkubwa ukiwa karibu na mshambuliaji mwenzake Kagere.

Meddie alikuwa injini katika mchezo huo kwani kocha Patrick Aussems alikuwa akiwasisitiza wachezaji wake wawe wanahakikisha mipira inafika miguuni kwa Kagere na kuweza kutupia wavuni.

Mabeki wa Sevilla walibidi kutumia kazi ya ziada katika kumzuia hasa katika kipindi cha pili, hilo liliwezekana hasa baada ya John Bocco kutolewa na nafasi yake kuingia Adam Salamba.