Abramovich atumia mamilioni kuwalipa makocha anaowafukuza

Muktasari:

Bilionea huyo wa Russia ametumia Pauni 92.9 milioni kulipa fidia za kuwafukuza makocha tangu alipokuwa mmiliki wa klabu ya Chelsea mwaka 2003.

London, England. Roman Abramovich ni mtu na pesa zake. Hawajawahi kufikiria hasara na ndio maana amekuwa akiajiri na kuwafuta kazi makocha huko kwenye kikosi cha Chelsea kiasi cha kumgharimu karibuni Pauni 100 milioni kwa kulipa fidia tu za kufukuza makocha.

Bilionea huyo wa Russia ametumia Pauni 92.9 milioni kulipa fidia za kuwafukuza makocha tangu alipokuwa mmiliki wa klabu ya Chelsea mwaka 2003.

Abramovich tangu alipoinunua The Blues kutoka kwa Ken Bates, makocha 11 wamekuja na kuondoka Stamford Bridge, huku bilionea huyo wa Russia akimwaajiri na kumfukuza Kocha, Jose Mourinho mara mbili tofauti.

Maurizio Sarri anaweza kuwa kocha wa 12 kufutwa kazi huko Stamford Bridge kwa dalili zinavyoelekea huku ikielezwa kwamba huenda baada ya Fainali ya Europa League dhidi ya Arsenal basi unaweza kuwa mwisho wake wa kuwa bosi wa The Blues huku akiwindwa na Juventus baada ya Max Allegri kufutwa kazi huko Turin.

Hivi ndivyo Abramovich alivyowalipa fidia makocha aliowafuta kazi Chelsea.

Antonio Conte – Pauni 9 milioni

Julai mwaka jana, bilionea Abramovic alichukua uamuzi wa kumfuta kazi kocha, Antonio Conte baada ya Chelsea kufanya hovyo kwenye Ligi Kuu England. Mtaliano huyo alifunguliwa mlango wa kutokea na nafasi yake kuletwa Mtaliano mwingine, Maurizio Sarri. Conte alienda mahakamani na baada ya purukushani na huku na huko, hatimaye ameshinda kesi na hivyo Chelsea ililazimishwa kumlipa fidia ya Pauni 9 milioni ikiwa ni mshahara wa mwaka mmoja uliokuwa umebaki kwenye mkataba wake huko Stamford Bridge.

Jose Mourinho – Pauni 8.3 milioni

Kocha mwenye maneno mengi, Jose Mourinho alirudi Stamford Bridge kwa mara pili kufanya kazi kwenye kikosi hicho cha The Blues. Maisha yalianza vizuri, Mourinho akawapa ubingwa Chelsea kwenye msimu wake wa kwanza, lakini msimu uliofuatia mambo yalikuwa magumu. Maji yalizidi unga hadi kufikia Desemba 2015, Mourinho alionyeshwa mlango wa kutokea yeye pamoja na benchi lake lote la ufundi. Kutokana na hilo, Abramovich alilazimika kumlipa Mourinho na benchi lake la ufundi fidia ya Pauni 8.3 milioni kutokana na kumfukuza kazi.

Roberto Di Matteo – Pauni 10.7 milioni

Mtaliano Roberto Di Matteo kwanza aliingia Chelsea akiwa kocha wa muda akichukua mikoba ya Andre Villas-Boas baada ya kutibua mambo kwenye kikosi hicho. Di Matteo akawapa Chelsea ubingwa wao wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa kocha wa mpito na kisha akapewa kibarua cha kudumu huko Stamford Bridge. Lakini, kufikia Novemba 2012, miezi michache tu tangu alipotoa kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Di Matteo akaonyeshwa mpango wa kutokea huko Stamford Bridge. Kwa kuwa mkataba wake ndio kwanza ulikuwa mbichi, jambo hilo lilimfanya Abramovich amlipe Di Matteo fidia ya Pauni 10.7 milioni kwa kumtimua kazi.

 

Andre Villas-Boas – Pauni 12 milioni

Baada ya kufanya vizuri huko FC Porto kama ilivyokuwa kwa Mreno mwenzake, Jose Mourinho, Andre Villas-Boas alipata dili la kwenda kuinoa Chelsea, Juni 2011. Lakini, hadi kufikia Machi 2012 maisha ya AVB yalifikia ukingoni huko kwenye kikosi cha Chelsea baada ya kuonyeshwa mlango wa kutokea. Kwa sababu kocha huyo alikuwa hata mwaka hajamaliza katika mkataba wake huko Stamford Bridge kitendo cha kufutwa kazi ilibidi kimgharimu pesa nyingi bilionea Abramovich kwa ajili ya kulipa fidia, ambapo AVB aliweka mfukoni Pauni 12 milioni kwa kufutwa kazi na Chelsea.

Carlo Ancelotti– Pauni 6 milioni

Mtaliano mwingine kwenye rekodi za ukocha katika kikosi cha Chelsea. Mambo yalikuwa matamu kwa Ancelotti katika siku zake za mwanzo huko Stamford Bridge. Alitua hapo Juni 2009, lakini ilipofika Mei 2011 maisha yake kwenye kikosi hicho yalifikia tamati. Mbaya zaidi, Ancelotti alikwenda kufutwa kazi ugenini katika mechi ya mwisho ya msimu dhidi ya Everton huko Goodison Park. Hata hivyo, aibu hiyo ya kufukuzwa ugenini haikumwacha patupu Ancelotti, ambapo mwisho wa yote alilipwa fidia ya Pauni 6 milioni na kwenda kuendelea na maisha yake mengine akimwaachia Abramovich timu yake na kuamua kumpa kazi AVB.

 

Luiz Felipe Scolari – Pauni 12.6 milioni

Baada ya kutamba na Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia 2002 na kubeba ubingwa huo, Abramovich alikuwa akivutiwa na kocha huyo na ilipofika Julai 2008 akampa kazi Mbrazili huyo kwenda kuinoa timu yake ya Chelsea. Lakini, kitu kibaya, Scolari alidumu kwenye kikosi cha Chelsea kwa miezi saba tu, Februari 2009 akaonyeshwa mlango wa kutokea huko Stamford Bridge. Hata hivyo, ndani ya miezi hiyo saba aliyofutwa kazi, Scolari alipiga pesa ya maana baada ya kulipwa fidia ya kufukuzwa kazi kiasi cha Pauni 12.6 milioni. Lucha nyepesi ya kusema ni kwamba Abramovich alikuwa akigawa utajiri kwa kufukuza makocha.

Avram Grant – Pauni 5.2 milioni

Baada ya Jose Mourinho kutibua mambo huko Stamford Bridge, Abramovich aliona sio kesi, akampa kazi Muisraeli, Avram Grant. Grant aliingia mzigoni Chelsea Septemba 2007, lakini ilipofika Mei 2008, kibarua kiliota nyasi, akaonyeshwa mlango wa kutokea huko Stamford Bridge. Hata hivyo, kocha huyo hakuondoa mguu wake Stamford Bridge mikono mitupu, kitendo cha kufukuzwa kilimwingiza Abramovich kwenye hasara kubwa kwa sababu ilibidi azame mfukoni kutoa Pauni 5.2 milioni kulipa fidia ya kuvunja mkataba wa Grant. Kocha Grant ameiongoza Chelsea kwenye mechi 54 na kushinda mechi 36, akitoka sare 13 na kupoteza mara tano na kufunga mabao 97 na kufungwa 36.

Jose Mourinho – Pauni 23.1 milioni

Akitokea Ureno kwenye kikosi cha FC Porto alikopata mafanikio makubwa, Juni 2004, Mourinho alipata dili la kazi kwenye kuinoa Chelsea kwenye Ligi Kuu England. Hapo ndipo alipojipachika jina la Special One. Lakini, kibarua chake hicho alidumu nacho kwa miaka mitatu tu, kwani ilipofika Septemba 2007, alionyeshwa njia ya kutokea kwenye kikosi hicho na kufunguliwa geti la kuto