Zahera aumia kuwaacha nyota wake waliovumia tabu Yanga

Muktasari:

Yanga imemaliza ligi ikiwa katika nafasi ya pili huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya Azam FC.

Dar es Salaam. Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema inamuwia vigumu kuachana na baadhi ya nyota kutokana na kukaa nao vizuri katika kipindi cha changamoto katika klabu hiyo.

Mchezo wa Azam FC na Yanga unaotarajiwa kuchezwa Juni 28, utakaotoa hatma ya nyota wanaobaki na wanaoondoka huku wengi wao wakiwa wamemaliza mikataba na klabu hiyo.

Zahera alisema wamemaliza vyema msimu pamoja na kupita katika kipindi kigumu lakini muda wa wao kuondoka unapofika unamyima raha kwani ni ngumu kuachana na mtu aliyemzoea na kuishi naye kwa wakati wote.

"Roho inauma na huwa nawaza kila siku sijui nianzie wapi na niishie wapi, lakini jambo hilo lipo na lazima lifanyike ili kutengeneza kikosi kizuri kwaajili ya ushindani, lakini kuhusiana na kumuacha mchezaji au kubaki naye kikosini ifikapo mwisho wa msimu ni ishu inayofanyika mara kwa mara mimi sitakuwa wa kwanza."

"Mimi naondoka Mei 28 usiku, kwahiyo wachezaji wote tunaowasajili msimu huu tutawatangaza tarehe hiyo. Wachezaji nane tayari wameshakubali, sita ni wa Kimataifa na wawili ni wa hapa ndani ukiona wapya wanaingia basi kunawanaotoka nieleweke ivyo lakini siwezi kusema sasa muda ukifika itafahamika", alisema Zahera.