Kawhi aibeba Raptors ikishinda ugenini dhidi ya Bucks

Muktasari:

Raptors sasa washindwe wenyewe kwenye mchezo ujao nyumbani endapo wakishinda watatinga fainali.

Dodoma. Siku chache baada ya kuombwa asiondoke na mashabiki wa timu ya Toronto Raptors, Kawhi Leonard ameiongoza timu hiyo kupata ushindi muhimu ugenini dhidi ya Milwaukee Bucks katika fainali ya mashariki.

Alfajiri ya kuamkia leo Ijumaa, Kawhi amefunga vikapu 35, asisti tisa na kupata ribaundi saba katika dakika 40 alizocheza na kufanikisha ushindi wa vikapu 99-105 waliopata dhidi ya wenyeji Milwaukee Bucks uwanja wa Fiserv Forum.

Mbali na Kawhi, wachezaji wenzake Fred VanVleet aliyefunga vikapu 21, Kyle Lowry 17 na Pascal Siakam 14 kwa pamoja walishiriki kupatikana ushindi huo muhimu ugenini mbele ya timu ngumu Milwaukee Bucks.

Staa wa Bucks anayetarajiwa kushinda tuzo ya MVP msimu huu, Giannis Antetokounmpo alifunga vikapu 24 pekee katika dakika 39 alizocheza wakati Eric Bledsoe alifunga 20, Malcom Brogdon 18 na Brook Lopez akifunga vikapu na 16 pekee wakishindwa kuitetea timu yao ikifungwa mchezo wa tatu mfululizo.

Kwa matokeo hayo Raptors wanaweza kumaliza kazi tofauti na matarajio ya wengi katika mchezo wa sita badala ya mechi saba kama watashinda mchezo wa Jumapili katika uwanja wake wa scoatiabank Arena.

Ushindi huo umempa mzuka shabiki 'lialia' wa Toronto Raptors, Mwanamuziki nyota Drake ambaye anaishi Toronto ilipo timu hiyo.

Kuonyesha kwamba ana mchango mkubwa ikiwemo hamasa na kuvutia watu mbalimbali kufanya matembezi kwenye timu hiyo, Rais wa timu hiyo Masai Ujiri alimzawadia koti maalum lenye thamani ya Sh1.7 Bilioni 1.7 Jumanne wiki hii.