JACOB MASSAWE: Nilimnasa mchezaji akiniroga - 2

Muktasari:

Makongamano yake ndiyo yamenifanya hivi nilivyo, bado yanaishi moyoni mwangu kwani alinifungua vitu vingi na ndiyo maana siwezi kutumia uchawi kwenye kazi zangu

Dar es Salaam. Katika sehemu ya kwanza ya makala haya na mchezaji kiraka wa Stand United, aliyetamba Ligi Kuu ya Bara kama kiungo, kisha beki na sasa straika, Jacob Massawe ‘Le Captain’, tuliangazia soka lilivyompa mke. Twende pamoja leo tena.

KILICHOMRUDISHA NDANDA
Massawe anasema ndani ya Stand United 'Chama la Wana', kulitokea mgawanyiko ambapo kuna viongozi ambao hawakuwa sawa naye.
"Napenda kutetea haki za wachezaji wenzangu baadhi ya viongozi waliniona nashawishi wenzangu kugoma, basi nikawa naongelewa vibaya, kama mwanadamu nikajisikia hovyo, nikaamua kurudi Ndanda ambako niliisaidia isishuke daraja kwani mechi ya mwisho ndiyo ilikuwa inaamua matokeo, tulicheza dhidi ya Mwadui FC, tulishinda mabao 3-0, mimi nilifunga mawili.
"Ndanda nako nilikuwa nahodha, lakini baadaye viongozi wa Stand United wakaniomba nirudi tena kuisaidia timu, hapo wakaniambia nitakuwa kocha msaidizi, mkuu alikuwa ni Nassor Masoud 'Chollo'.
"Kocha alikuwa Patrick Liewig akamtoa Chollo akanipa mimi kuwa nahodha mkuu na msaidizi wangu akawa Amri Kiemba, alinitia moyo na kwamba nisiangalie mafanikio yake bali nifanye kazi."
"Awamu hiyo ilikuwa ngumu sana kwangu kwani, nilikuwa nawaza namna ya kuwaongoza mastaa ambao walikuwapo ndani ya timu kama Elias Maguli, Abuu Ubwa, Haruna Chanongo, Kiemba, Zahiri na Chollo, nilichokifanya nikamsoma mmoja baada ya mwingine bila wao kujijua kisha nikawa naishi nao kwa akili," alisema.

MAHUBIRI YAMEMBADILISHA
Muonekano wa Massawe ni mchezaji mwenye nidhamu na mnyenyekevu, kumbe alivyo imetokana na jinsi ambavyo alikuwa anamfuatilia mhubiri wa kimataifa, mwalimu Christopher Mwakasege. "Makongamano yake ndiyo yamenifanya hivi nilivyo, bado yanaishi moyoni mwangu kwani alinifungua vitu vingi na ndiyo maana siwezi kutumia uchawi kwenye kazi zangu," anasema.

MAOMBI YAKE YAMUUMBUA MCHAWI
Anafichua siri ambayo alikaa nayo kimya kwa muda mrefu kwamba wakati anaichezea Ndanda FC, kuna mchezaji alikuwa anacheza naye namba moja, alimkamata akimfanyia ushirikina.
Anasimulia kwa machungu makubwa: "Nilikuwa napata maumivu makali bila kuumia mazoezini wala kwenye mechi, maisha yangu Ndanda yalikuwa ya shida kupita kiasi bila kuchomwa sindano ya ganzi ama kumeza dawa uwanjani nisingekuwa naingia kucheza.
"Nikimaliza mechi nilikuwa silali nalalamika usiku kucha, daktari akiniangalia anaona sina tatizo lolote, kwenye mpira kuna uchawi asikuambie mtu, baadae likanijia wazo la kufunga na kuomba hapo ndipo nilipoona vitu vya kutisha.
"Nilionyeshwa kuna mchezaji ambaye siwezi kumtaja jina kwa kumtunzia heshima yake, kisha nikamfuata na kumueleza aache kuniloga nashukuru Mungu alinielewa na akaniomba msamaha.
"Kwa sasa amekuwa rafiki yangu mkubwa ambaye tunashauriana vitu vingi, ukweli ndani ya soka kuna ushirikina wa ajabu na siyo kila mchezaji mwenye majeraha hazingatii miiko ya soka, hata vitabu vya dini vimeandika kuna wachawi na siyo kwenye mpira wa miguu tu nadhani katika kazi mbalimbali wengi wanakumbana na haya," anasema.

BILO AMEMPA MAFANIKIO
Baada ya Stand United kuwa chini ya kocha, Athuman Bilali 'Bilo', Massawe amebadilishiwa majukumu anacheza nafasi ya ushambuliaji na tayari ametisha katika mafasi hiyo akitupia mabao 10 mpaka sasa.
"Kati ya nafasi ambazo nimeona imeweza kunitoa basi ni hii ambayo nacheza sasa na kama ningeanza nayo msimu kadhaa nyuma ningekuwa kwenye kinyang'anyiro cha ufungaji bora na hao kina Meddie Kagere," anasema.

YANGA AMEIFUNGA SANA
Anasema amekuwa na bahati ya kuifunga Yanga katika kila timu ambayo amewahi kuichezea. "Japokuwa matokeo tulikuwa tunafungwa wakati mwingine 2-1 lakini mimi ndiye nilikuwa nafunga, ushindi ni huu ambao niliwafunga nikiwa na Stand.
Vipi kuhusu kuifunga Simba? Anajibu:  "Sijabahatika kuwafunga Simba ingawa nikiwa ndani ya uwanja wenzangu ndiyo waliifunga, lakini ipo siku nitawafunga tu na wao," anasema.  

ANA MJENGO
Mbali na soka kumfanya apate mke, pia amejenga mjengo wa maana mkoani kwao Shinyanga ambayo anaishi na familia yake. "Ninaishi kwangu nashukuru Mungu, lakini pia nina nyumba ya biashara ambayo nimeweka wapangaji, naamini hata gari nitanunua tu kila jambo lina hatua zake," anasema.

MAISHA NJE YA UWANJA
Wadau wengi wa soka wanamfahamu Massawe akiwa ndani ya uwanja, lakini anafichua ni mtu wa aina gani anaporejea kwenye familia yake kwamba anapenda kumsaidia mke wake kufanya kazi za nyumbani.
"Nikirejea nyumbani basi mke wangu anapata raha, kasoro kupika tu ndiyo sijui ila mambo ya usafi hapa ndiyo mwenyewe, nampenda kwa sababu anajitambua na msikivu na ndiye aliyenishawishi kushika dini," anasema.