Wanazingua! Warembo wa Bongo wanapotea hapa tu

Muktasari:

Unajua kama Wema Sepetu aliwahi kuendesha mjini, Audi Q7? Gari la Sh250 milioni. Jiulize kwa sasa anatumia usafiri gani? Huo ndiyo mfano wa warembo mastaa. Hawana tofauti na Apolo. Wakipatia chaneli wanatesa si polepole. Chaneli ikiingia chenga, msoto kama kawa.

Dar es Salaam.Leo hana hata shing’mia, kesho milionea na anatesa viwanja mpaka unamuogopa. Leo anamiliki magari, pikipiki na hata majumba, kesho hana kitu. Amekaukiwa kabisa. Hayo ndiyo maisha ya Apolo, kwenye machimbo ya Tanzanite, Mererani, Simanjiro kule Manyara.

Miaka mitatu iliyopita nilitembelea Mererani. Nikakutana na Apolo wapo mawindoni. Huingia shimoni saa 24 kwa siku. Yaani mtu unaingia kwenye handaki leo muda huu, unatoka kesho saa na dakika kama hizi. Unaambiwa migodi mingine watu wanazama saa 48. Pesa zinatafutwa.

Baadhi ya Apolo niliwafanya washkaji. Nikapiga nao stori. Wakaniambia kuwa Apolo kuishi miezi ama mwaka bila kushika hata Sh10,000 ni jambo la kawaida. Wapo ambao wamesota miaka 10 hawajawahi kupata jiwe la ushindi. Wanaendelea kukomaa kwa matumaini.

Wapo ambao wanapambana hata buku hawana. Ukimuuliza anakwambia aliwahi kupata jiwe akauza Sh50 milioni. Hata hivyo, baada ya muda pesa hizo zote ziliisha, kisha akarejea mgodini kuzisaka upya.

Wapo waliniambia: “Mwanangu unaona life lilivyo ngumu hapa, ghafla unapata zali, unakutana na jiwe unauza milioni 20, hapo lazima utese kimtindo, upunguze machungu ya msoto. Hivyo ndivyo pesa huondoka.”

Mererani kuna watu huenda kununua nyumba, magari na pikipiki kwa bei chee. Apolo wakinasa mawe na kutengeneza fedha, hununua magari na nyumba. Wakiishiwa huuza kwa bei rahisi.

Nyumba yenye thamani ya Sh50 milioni, Apolo anaweza kuiuza Sh15 milioni pale anapoishiwa. Wanajua sana kula bata, ila pia wanafahamu maana ya kuzitafuta pesa. Usimuone kachoka leo na mavumbi yake, kesho unaweza kumkuta anatumia jasho lake Naura Spring na usimtambue.

KAMA WAREMBO MASTAA

Lifestyle ya Apolo, leo kachoka kesho milionea mwenye kula bata, ipo sawa na warembo mastaa Bongo. Aisee, leo utamuona anakokota mkoko wa bei mbaya na utaogopa, kesho pesa ya kuita Uber ni mtihani.

Unajua kama Wema Sepetu aliwahi kuendesha mjini, Audi Q7? Gari la Sh250 milioni. Jiulize kwa sasa anatumia usafiri gani? Huo ndiyo mfano wa warembo mastaa. Hawana tofauti na Apolo. Wakipatia chaneli wanatesa si polepole. Chaneli ikiingia chenga, msoto kama kawa.

Kwani wewe ulikuwa wapi wakati ule Wema anatangaza kununua mjengo wenye thamani ya Sh400 milioni? Mjengo upo Kijitonyama, Dar. Mwaka 2016, Wema aliuacha mjengo kama ulivyo na kuhamia Ununio, Da! tena kupanga.

Je, mjengo wa K’nyama aliuongopea umma kuwa aliununua? Vipi, aliuuza baada ya mambo kumwendea mrama? Kwa ufupi hiyo ndiyo hali halisi ya mastaa wa kike. Maisha yao kama bahari. Mara kupwa, mara kujaa!

Ulikuwa mjini wakati huo Wema anamleta staa wa Nollywood, Omotola Jalade kuzindua filamu yake? Wakati huo kampuni yake ya Endless Fame ikiwa ‘on fire’, ikitoa ajira kadhaa kwa majanki wa Bongo Movie. Mara tukasikia jamaa fulani aliyewekeza mapene yake kwake alikwenda ofisini kwa Wema, Mwananyamala na kukomba zaga zote. Ni baada ya mambo flani ya nahii kuleta mishikeli.

Ulikuwa unamiliki simu yenye intaneti kipindi Wema anapewa na Diamond Platnumz, zawadi ya gari aina Nissan Murano kwenye birthday yake? Siku hiyohiyo, mshefa mwingine akamnunulia Wema BMW. Meneja wake, Martin Kadinda akakabidhi. Akaongopa kuwa yeye ndiye kanunua.

Jiulize magari yote hayo yamekwenda wapi? Kwa taarifa yako ni kuwa mgongano huo wa zawadi za magari ndiyo ulisababisha Diamond ajiondoe kwa Wema. Alishtukia kuna kidume kingine kilinunua BMW. Mondi akaona hana chake.

Usisahau Wema ndiye aliyemtoa jela Kajala Masanja. Kipindi hicho ushosti umekolea kweli. Kajala alihukumiwa jela miaka mitano au faini Sh13 milioni. Wema akawaambia askari magereza pale Mahakama ya Kisutu, wasimpeleke jela, wamngoje aende ‘kudroo’ pesa benki. Wema alifanikisha.

Kabla ya Diamond kumiliki BMW X6, ndinga kama hiyo ilimilikiwa na supastaa Jacqueline Wolper. Mkoko wa Sh200 milioni. Wakati huo Jackie wa moto sana. Marehemu Sajuki alipokuwa anaumwa, alihitaji msaada wa hali na mali. Jackie alimtembelea Sajuki na kumkabidhi Dola 10,000, sawa na Sh16 milioni kwa wakati huo.

Baada ya miezi sita, Jackie hakuwa na X6 tena, hata hayo mamilioni hakuwa nayo. Akarejea kwenye maisha ya kawaida. Nani alikuwa anampa jeuri yote? Sioni umuhimu wa kumtaja. Hata hivyo, somo ni lilelile kuwa mastaa wa kike kuna wakati huwa watamu kiuchumi mpaka utawaogopa, ila sometimes wanakaa juu ya mawe mpaka wanakumbuka mikwanja waliyoitekeza nyakati za ukwasi.

Hivi unainyaka kuwa Aunty Ezekiel kuna kipindi alikuwa pedeshee? Wakati huo anaitwa Mrs Pemba. Alikuwa akiishi na mtu mbaya Jack Pemba kama mke na mume. Jack alivyo mtu wa matanuzi na matumizi. Mpaka bendi ziliwaimba Jack Pemba na Aunty Pemba. Nini kilifuata? Walipoachana, Aunty aliyarudia maisha yake.

Irene Uwoya matata sana yule mtoto wa kike. Binti mdogo mambo makubwa. Ungemuona ndani ya Toyota Fortuner, muziki mnene, kila siti ina kideo. Mtoto anashusha vioo mpate kumuona vizuri akiendesha na msikie sawia mdundo mkubwa wa muziki. Unadhani lile gari lilikwenda wapi?

Siku nyingine utamuona kwenye gari lingine la bei ya kawaida au amedandia lifti. Kuna wakati utasikia anafanya ziara Ulaya na Marekani kuliko Waziri wa Mambo ya Nje, halafu zitapita nyakati hasikiki kabisa. Amepoa, mbwembwe zote kwisha. Maisha yao yapo kisinema sana!

Unaikumbuka ndoa ya Aunty na Sunday Demonte? Sherehe ikafanyika Dubai. Wakati huo Aunty alikuwa bosslady kama Zari. Jacob Stephen ‘JB’, Steve Nyerere na Ray Kigosi walikwea anga kwenda kuhudhuria shughuli kwa gharama za Aunty.

Demonte alipofungwa Falme za Kiarabu, mambo yakageuka juu chini. Aunty akajituliza kwa dansa wa WCB, Mose Iyobo. Inasemekana Demonte alishatoka jela, lakini mambo si kama zamani. Na ndoa imebaki stori tu.

Hili ni jicho tu la mshangao. Mara wanachanua na kupendeza kama maua saa sita wakati wa jua la utosi, kipindi kingine huwaoni wakiushika mji. Wanakuwa wapole.

Kuna mrembo staa acha nimhifadhi jina. Miaka michache iliyopita aliwahi kunichamba nikachambika, kisa nilimpa dili ambalo pesa yake aliiona mbuzi. Alikuwa na fedha nyingi sana wakati huo. Nikaachana naye, nikamsogezea mwenzake dili hilo, mambo yakaenda vizuri. Biashara ilifanyika.

Mwaka uliofuata, yule staa aliyenichamba kisa dili la hela ndogo, alinifuata mwenyewe ili nimuunganishie dili lilelile. Sikuwa na kinyongo. Nilimuunganisha. Akawa mtiifu na kutekeleza vigezo na masharti. Ooh, hapo alikuwa ameshaishiwa na kukumbuka michongo aliyoikataa siku za nyuma alipokuwa wamo. Vipi, wana tofauti na Apolo?