Samatta: Nitastaafia soka Mamelodi Sundowns bondeni

Muktasari:

Baada ya misimu mitano ya kucheza Mazembe hatimaye alitua Genk ya Ubelgiji ambako anatamba mpaka sasa

Dar es Salaam.Katika Bara la Afrika, Samatta amechezea klabu nyingi za Tanzania zikiongozwa na Simba ya jijini Dar es Salaam. Kabla ya hapo aliwahi kucheza timu ya utotoni ya Kimbangulile, akacheza Mbagala Market ambayo baadaye ilibadilishwa kuwa African Lyon. Baadaye akatua Simba.

Hakucheza sana Simba. Ndani ya msimu mmoja kamili alikuwa ameuzwa kwa shilingi 150 milioni kwenda TP Mazembe akiwa mchezaji wa kwanza ghali katika soka la Tanzania. Baada ya misimu mitano ya kucheza Mazembe hatimaye alitua Genk ya Ubelgiji ambako anatamba mpaka sasa.

Endapo mambo yataenda sawa, Samatta anaweza kwenda England katika dirisha hili. Huku ni kuendelea kupanda kwa Samatta. Lakini kama ilivyo kwa mastaa wengi wa soka, umri ukizidi kwenda juu ipo siku ambayo kiwango chake kitaanza kushuka na atatumia ngazi hiyo hiyo aliyopandia kushuka chini.

Namuuliza Samatta ni klabu gani ya Afrika ambayo angetamani kumalizia maisha yake ya soka. Jibu la Samatta linashangaza kidogo. Ungeweza kudhani ataitaja Simba ambayo ipo ardhi ya kwao. Ungeweza kudhani angependa kustaafia TP Mazembe ambayo ilimkuza kimataifa. Lakini Samatta anakuja na jibu tofauti.

“Kwa muda mrefu nafikiria kama nikirudi Afrika kucheza soka, basi nigependa kucheza Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini na kustaafia hapo. Sijui kwanini lakini ningependa sana kucheza ile timu na ningependa kucheza soka la Afrika Kusini kwa ujumla,” anasema Samatta.

“Jamaa nasikia wapo vizuri na nasikia wana pesa pia. Wameziweka pembeni zile klabu zao kubwa (Orlando Pirates na Kaizer Chiefs). Huwa nawakubali sana na ningependa kulionja soka lao siku moja nikianza kuwa mzee,” anaongeza Samatta.

Baada ya maongezi mengi na Samatta, huku nikiwa na taarifa kwamba anaweza kuondoka Genk katika dirisha hili, Samatta anaelezea kumbukumbu zake kadhaa klabuni hapo. Namuuliza ni bao gani ambalo atalikumbuka zaidi Genk na ananijibu kwa upole tu.

“Nimefunga mabao mengi lakini bao ambalo naweza kusema nalikumbuka sana ni bao langu la kwanza. Halikuwa bao zuri sana kwa maana ya uzuri wa ufungaji wenyewe kwa sababu niliugusa tu mpira ukaingia wavuni,” anasema Samatta.

“Lilikuwa bao langu la kwanza Ulaya na lazima ujisikie vizuri. Nakumbuka nilifunga katika uwanja wa nyumbani. Mimi ni mshambuliaji kwahiyo lazima ujisikie vizuri unapofunga hasa bao lako la kwanza,” anasema Samatta.

Kwa sasa Samatta amezunguka katika viwanja vikubwa barani Ulaya katika michuano ya Europa. Hii ni kutokana na kucheza na klabu kubwa za Ulaya kama vile Besktas, Atheltic Bilbao, Rapid Viena na nyinginezo. Lakini hata hivyo anauvulia kofia zaidi uwanja mmoja.


“Nimecheza viwanja vingi vikubwa. Kuna ule wa Atheltic Bilbao (San Memes), Rapid Vienna (Allianz Stadion), kuna ule wa Besiktas (BJK Vodafone Park) lakini hata hivyo, ule Uwanja wa Besiktas ni kiboko aisee. Jamaa wana kelele sana. Unashindwa hata kuwasiliana na mchezaji mwenzako. Ule ndio uwanja ambao unasikia filimbi nyingi na wala haujui ya mwamuzi ni ipi. Hata hivyo, nilifunga mabao mawili pale,” anasema Samatta.

Samatta anatoa tofauti kubwa kati ya mashabiki wa soka la Ulaya na wale wa soka la Tanzania. Anaamini kwamba Tanzania hakuna mashabiki bali kuna watazamaji. Watu wanaokwenda uwanjani na kutulia tu.

“Tanzania hakuna mashabiki brother. Kuna watazamaji tu. mtu anafika uwanjani anakaa chini anatazama tu mpira. Ulaya ndio kuna mashabiki. Si unaona upande ule kule (ananionyesha upande wa mashabiki ‘vichaa’ wa Genk) kuna watu kwanza hawakai, halafu kuna watu hawatazami mpira wao kazi yao ni kuwageukia wenzao na kushangilia huku wakihamasisha kushangilia,” anaongeza Samatta.

“Pale Mazembe kuna wale mashabiki wanaitwa Mia kwa Mia. Nao ni washangiliaji wazuri sana hauwezi kuwafananisha na mashabiki wetu nyumbani. Watu inabidi wabadilike sana aisee,” anaongeza Samatta.

Wakati wimbo wa Samagoal ukitamba kwa sasa Ulaya, Samatta alishakuwa na nyimbo kadhaa pale Mazembe. Anaamini sio kila mchezaji anatungiwa nyimbo, bali inatokana na juhudi za mchezaji binafsi uwanjani.

“Kwa mfano hapa Genk sio kila mchezaji ana wimbo. Ni mimi tu ndiye ambaye ninaimbwa. Inatokana na jinsi ambavyo nimewaridhisha mashabiki na ndio maana huwa wanafanya hivyo. Kwa wenzetu ni namna ya kunyanyua morali yako,” anaongeza Samatta.

Tunafika mwisho wa mazungumzo yetu na Mbwana Samatta. Ni mara ya tatu Mwanaspoti limefanikiwa kufanya mahojiano na staa huyu wa kimataifa wa Tanzania anayecheza kwa mafanikio klabu ya Genk akiwa nyumbani kwake Ubelgiji. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2012 wakati alipotua TP Mazembe. Mwanaspoti ilimfuata mpaka Lubumbashi. Mara ya pili ilikuwa Aprili 2016 miezi miwili baada ya kujiunga na klabu yake ya sasa Genk. Hii ni mara ya tatu.

Shukrani kubwa kwa Samatta mwenyewe ambaye amekuwa akitoa ushirikiano wa mara kwa mara kwa waandishi wetu akiwa ndani ya Tanzania na nje ya Tanzania. Tutaendelea kushirikiana naye bega kwa bega.