Viwanja na Miji itakayobamba AFCON Misri

Muktasari:

Timu hizo 24 zinatarajia kutumia jumla ya viwanja sita ambavyo vipo katika miji minne tofauti kusaka ufalme wa Bara la Afrika kwa mwaka huu ambao mshindi wake atazawadiwa kitita cha Dola 4 milioni (Shilingi 9.2 bilioni)

Dar es Salaam. Muda unazidi kuyoyoma na Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) ambazo mwaka huu zitafanyikia Misri zinazidi kujongea na ukipiga hesabu vizuri ni wazi kwamba utapata jibu kuwa zimebaki siku 29 kabla ya kuanza kwa mashindano hayo ambayo pazia lake litafunguliwa rasmi Juni 21 huko Misri.
Historia mpya itaandikwa kupitia mashindano ya mwaka huu kwani kwa mara ya kwanza yatashirikisha jumla ya nchi 24 ambazo tayari zimeshapangwa kwenye makundi sita (6) na baada ya hatua ya makundi, kutakuwa na hatua ya robo fainali kisha nusu fainali na baadaye mechi ya kuwania mshindi wa tatu na hatua ya fainali.
Timu hizo 24 zinatarajia kutumia jumla ya viwanja sita ambavyo vipo katika miji minne tofauti kusaka ufalme wa Bara la Afrika kwa mwaka huu ambao mshindi wake atazawadiwa kitita cha Dola 4 milioni (Shilingi 9.2 bilioni).
Kuelekea fainali hizo ambazo pia timu ya taifa ya TANZANIA 'Taifa Stars' itashiriki ikipangwa kundi C, gazeti hili linakuletea dondoo fupi za viwanja na miji ambayo itatumika kwa fainali hizo za 32 za Mataifa ya Afrika.

1.Uwanja wa Kimataifa wa Cairo (Cairo)
Kati ya viwanja vyote sita ambavyo vitatumika kwenye fainali hizo, Uwanja wa Kimataifa wa Cairo ambao upo jijini Cairo ndio mkubwa zaidi ukiingiza idadi ya mashabiki 75,000 ukiwa na hadhi ya Olimpiki na eneo lake la kuchezea lina nyasi za asili na ulifunguliwa rasmi Julai 23, 1960.
Mhandisi msanifu wa Uwanja huo ni Mjerumani Werner March ambaye pia ndiye aliyesimamia ujenzi wa Uwanja wa Olimpiki wa Berlin huko Ujerumani.
Uwanja huo wa Kimataifa wa Cairo, upo umbali wa Kilomita 10 Magharibi mwa jiji hilo na umekuwa ukitumiwa na timu ya Taifa ya Misri pamoja na klabu za Zamalek na Al Ahly.
Kwenye AFCON utatumika kwa mechi 10 ambazo ni tano za hatua ya makundi, mechi mbili za hatua ya 16 bora fainali, moja ya robo fainali, moja ya nusu fainali na mchezo wa fainali.

2.Uwanja wa Juni 30 (Cairo)
Uwanja huo ambao unamilikiwa na Kikosi cha Anga cha Jeshi la Misri, utahodhi jumla ya mechi 10 kwenye fainali za AFCON ambapo kati ya hizo, saba ni za hatua ya makundi, mmoja wa hatua ya 16 bora, mchezo mmoja wa robo fainali na nusu fainali.
Ni wa nyasi bandia ambao unaingiza jumla ya mashabiki 30,000 na ulifunguliwa rasmi Julai 2,2012 na umekuwa ukitumiwa ka klabu ya Pyramids FC kuchezea mechi zake za nyumbani.

3.Uwanja wa Al Salam (Cairo)
Ulifunguliwa rasmi mwaka 2009 na unaingiza jumla ya mashabiki 30,000 na kwenye mashindano ya AFCON, jumla ya mechi 10 zitachezwa kwenye uwanja huo ambapo kati ya hizo, saba ni za hatua ya makundi, moja ya hatua ya 16 bora, moja ya robo fainali na mchezo wa kuwania mshindi wa tatu.
Uwanja huo wenye nyasi za asili unatumiwa na timu za El Entag El Harby na Al Ahly.

4.Uwanja wa Suez (Suez)
Ni Uwanja wa nne kwa kuingiza idadi kubwa ya mashabiki kati ya sita zitakazotumika kwenye fainali hizo ukiingiza jumla ya watu 27,000 na unatumia nyasi za asili na ulifunguliwa rasmi mwaka 1990 ukitumiwa na klabu za  Asmant El-Suweis na Petrojet.
Mechi nane zitachezwa kwenye Uwanja huo ambapo sita ni za hatua ya makundi, moja ya hatua ya 16 bora na nyingine moja ni ya robo fainali.

5.Uwanja wa Alexandria (Alexandria)
Moja ya viwanja vikongwe vya soka nchini Misri ukiwa umefunguliwa mwaka 1929 na kwa sasa unaingiza jumla ya mashabiki 20,000 walioketi kwenye viti huku ukitumiwa na klabu za Al Ittihad na Smouha na una nyasi za asili.
Utumika kwa mechi tano za hatua ya makundi na mechi mbili za hatua ya 16 bora.

6.Uwanja wa Ismailia
Ni Uwanja wenye nyasi za asili uliopo jijini Ismailia ambako unatumiwa na klabu ya Ismailia inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo na unaingiza mashabiki 18,525.
Utatumika kwa mechi saba ambapo sita ni za makundi na moja ya hatua ya 16 bora.