Bocco, Kagere wafunika Taifa, Sevilla yaichapa Simba

Muktasari:

Achana na matokeo ya mchezo huo matukio kadhaa yaliyojitokeza ndani na nje ya uwanja, kiwango bora cha Simba dhidi ya Sevilla ya Hispania ni ishara tosha ya ubora wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Dar es Salaam. Mabao ya washambuliaji John Bocco na Meddie Kagere yameshindwa kuisaidia Simba kukwepa kipigo cha magoli 5-4 kutoka kwa Sevilla katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo ulidhamiwa na Sportpesa, mabingwa wa Tanzania Bara, Simba ilianza kwa kishindo na kufanikiwa kwenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 3-1, lakini hali ilibadilika baada ya mabadiliko ya kipindi cha pili na kuwaacha Wahispania hao kusawazisha na kushinda 5-4.

Achana na matokeo ya mchezo huo matukio kadhaa yaliyojitokeza ndani na nje ya uwanja, kiwango bora cha Simba dhidi ya Sevilla ya Hispania ni ishara tosha ya ubora wa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Licha ya kufungwa mabao 5-4, Simba ilionyesha kiwango bora hasa nahodha John Bocco ambaye alifanya kazi nzuri katika eneo la ushambuliaji.

Pamoja na muda mfupi waliopata kujiandaa na mchezo huo na uchovu walionao baada ya kucheza mechi nyingi mfululizo kwenye Ligi Kuu, Simba ilithibitisha kuwa waandaaji wa mechi hiyo ya kimataifa ya kirafiki hawakukosea kuwapa nafasi ya kupambana na Sevilla ambao ni mabingwa wa kihistoria wa mashindano ya Europa Ligi.

Soka la kasi, pasi fupi na uharaka wa wachezaji wa Simba katika kufanya uamuzi pindi wawapo na mpira, vilitosha kuitikisa Sevilla katika mchezo huo tofauti na matarajio ya wengi kuwa timu hiyo ingekutana na urahisi katika mchezo huo.

Ingawa katika hali ya kawaida, ilitegemewa Simba iingie kwa mbinu ya kuzuia kutokana na ubora wa mchezaji mmoja mmoja wa Sevilla kulinganisha na wao, hadithi ilikuwa tofauti na waliamua kuwapa mshituko wageni wao kwa kupishana nao ndani ya uwanja wakicheza kwa kufunguka na kushambulia bila hofu.

Wakianza na viungo watatu ambao wanasifika kwa kupiga pasi na kuchezesha timu, Simba ilimudu kuipa presha safu ya kiungo ya Sevilla iliyoongozwa na kiungo mzoefu Ever Banega na kuwafanya wasicheze kwa uhuru jambo lililoifanya timu hiyo ishindwe kutengeneza nafasi.

Kuanzia dakika ya mwanzo ya mchezo, ari ya wachezaji wa Simba ilionekana kuwa juu na walicheza kwa kujituma na jitihada hizo zilizaa matunda mapema dakika ya tisa baada ya kupata bao lililofungwa na John Bocco aliyeunganisha vyema pasi ya Meddie Kagere kufuatia shambulio la Simba lililoanzishwa na beki Zana Coulibaly.

Baada ya kuingia bao hilo, Simba ilichangamka na kuendelea kucheza kwa kasi na kupeleka mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Sevilla na ilipata bao la pili kupitia kwa Kagere dakika ya 16 baada ya kunasa pasi ya nyuma ya beki Sergi Gomez aliyeghasiwa na Clatous Chama.

Makosa ya wachezaji wa Simba kushindwa kuokoa mpira katika eneo lao kupitia shambulizi la kona iliyochongwa langoni mwao, yaliwaponza dakika ya 28 baada ya Sevilla kupata bao la kwanza kupitia kwa beki Sergio Escudero, aliyemalizia mpira uliowababatiza mabeki wa Simba na kumfikia mguuni.

Hata hivyo, bao hilo la Sevilla halikudumu muda mrefu kwani dakika nne tu baadaye, Bocco alifunga bao la tatu akiunganisha vyema pasi ya Kagere kufuatia shambulizi la kushtukiza baada ya kupoka mpira kutoka kwa wapinzani wao.

Matokeo hayo yalidumu hadi filimbi ya mapumziko ilipopulizwa na mwamuzi Hery Sasii.

Kipindi cha pili Simba iliwatoa Pascal Wawa na Emmanuel Okwi na nafasi zao zilichukuliwa na Yusuph Mlipili na James Kotei.

Sevilla iliwatoa Jesus Navas, Franco Vazquez, Simon Kjaer, Wissam Ben Yedder, Sergio Escudero, na Roque Sema na nafasi zao zilijazwa na Bryan Gil, Aleix Vidal, Munir El Haddadi, Ibrahim Amadou na Joris Gnagnom.

Sevilla ilipata bao la pili kupitia kwa Nolito aliyeunganisha vyema pasi ya Gil. Simba ilifunga bao la tatu kupitia kwa Chama aliyepata pasi ya Bocco.

Simba pia iliwatoa Haruna Niyonzima, Jonas Mkude Chama, Bocco na Mohammed Hussein na Hassan Dilunga, Mzamiru Yassin, Adam Salamba, Rashid Juma na Mohammed Ibrahim. Simba ilichapwa bao la tatu dakika ya 84 lililofungwa na Quincy Promise na bao la kusawazisha kupitia kwa Munir El Haddad kabla ya Nolito kupiga bao la ushindi.

Simba: Aishi Manula/Deo Munishi, Zana Coulibally, Mohammed Hussein, Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Jonas Mkude, Clatous Chama, Haruna Niyonzima, John Bocco, Meddie Kagere na Emmanuel Okwi.

Sevilla: Juan Soriano, Jesus Navas, Sergio Escudero, Simon Kjaer, Sergi Gomez, Ever Banega, Roque Sema, Wissam Ben Yedder, Manuel Nolito na Franco Vazquez.