Makambo apiga bao, awaaga mashabiki wa Yanga

Muktasari:

Mshambuliaji Makambo amekuwa na rekodi nzuri katika msimu huu akifunga mabao 17 na kuisaidia Yanga kumaliza katika nafasi ya pili

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo amegeuka lulu kwa mashabiki wake waliokuwa na hamu ya kuaga baada kufunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Baada ya filimbi ya mwisho Makambo alikwenda moja kwa moja katika jukwaani ya Uwanja wa Uhuru na kupiga picha (selfie) kwa kutumia simu za mashabiki wa timu hiyo ikiwa ni ishara ya kuwaaga.

Jambo lililofanya mashabiki hao kushangilia kwa nguvu Makambo makambo… huku wengine wakipaza sauti kumtakia kila la heri katika maisha yake ya soka.

Makambo alifunga bao hilo la ushindi kwa kichwa akiunganisha krosi ya beki wa kushoto Haji Mwinyi na kuifanya Yanga kuibuka na ushindi wa 1-0.

Makambo alisema anaondoka Yanga mwisho wa msimu huu na kuna mambo mengi ambayo atayakumbuka katika kikosi cha timu hiyo kwa muda wa mwaka mmoja ambao alioishi hapo licha ya kuwa ndio mara yake ya kwanza kufika Tanzania.

"Kwanza nitawakumbuka wapenzi na mashabiki wa timu yetu kokote ambapo timu ilipokuwa inacheza na wao walikuwepo, lakini wamekuwa wakiungana nami na kuwa pamoja katika muda wote niliokaa hapa Yanga tangu nafika mpaka naondoka," alisema.

"Sitaweza kuwasahau wachezaji wenzangu kwani tulikuwa tunashirikiana nao kwenye shida na raha mpaka timu nyingine imeniona, kocha wangu Mwinyi Zahera naye ni mtu wa kumshukuru katika maisha yangu ya hapa Yanga kwani amehusika kunifanya nionekane na timu nyingine kwa kunipa nafasi ya kucheza mara kwa mara.

"Kiongozi mwingine ambaye alikuwa nami bega kwa bega tangu siku ya kwanza hapa Tanzania na nitakuwa namkumbuka huko niendapo ni Ofisa habari msaidizi Godlisten Anderson 'Chicharito' alikuwa akipambana nami katika nyakati zote nilizokuwa napitia," alisema Makambo.

Makambi baada ya kuifungia Yanga bao pekee dhidi ya Mbeya City, alikwenda moja kwa moja katika moja ya majukwaa ya Uwanja wa Uhuru na kupiga picha (selfie) kwa kutumia simu za mashabiki wa timu hiyo ikiwa ni ishara ya kuwaaga.