Boban apewa mikoba ya Ajibu, Yanga yaichapa Mbeya City

Muktasari:

Endapo Ajib atakosekana, nafasi ya nahodha mara nyingi inakuwa ya Andrew Vicent 'Dante' au Juma Abdul ambao katika mchezo wa leo hawajapangwa.

Dar es Salaam.Kiungo wa Yanga, Haruna Moshi ‘Boban’ amepewa mikoba ya nahodha Ibrahim Ajib na kuiongoza timu hiyo kushinda bao 1-0 dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, kocha Mwinyi Zahera alimpa jukumu la unahodha Boban aliyejiunga na Yanga msimu huu wa katika dirisha dogo.

Boban amepewa mikoba ya Ajibu ikiwa ni siku moja tangu ilipovuja taarifa kuwa nahodha atajiunga bure na mabingwa wa DR Congo, TP Mazembe mwisho wa msimu huu.

Ajib anamaliza mkataba wake wa miaka miwili na Yanga unaofikia tamati Juni 30, 2019.

Mazembe imewaandikia barua Yanga kuwajulisha kuwa watamchukua Ajib rasmi Julai mosi 2019 na kwamba kama kuna utofauti wowote wa taarifa hiyo Yanga iwasiliane nao kwa mujibu wa Kanuni za Usajili za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

 

Katika dili hilo Yanga ni wazi haitapata fedha zozote kutokana na usajili huo kufuatia Ajib kuchukuliwa akiwa amemaliza mkataba lakini pia akimaliza uvumi wa kurejea Simba.

Simba ilikuwa inatajwa kutamani kumrudisha Ajib katika klabu yake ya zamani, lakini sasa Mazembe imemaliza rasmi uvumi huo.

Ajib anaweza kuwa mchezaji mapema kusajiliwa na Mazembe baada ya mmiliki wa klabu hiyo Moise Katumbi wiki hii kurejea nchini kwake baada ya kukaa uhamishoni kwa miaka kadhaa huku msimu Mazembe wakifanikiwa kuwa Mabingwa wa Ligi Kuu nchini DR Congo.