Mashabiki wa Yanga waisusa timu yao Uwanja wa Uhuru

Muktasari:

Yanga imeshindwa kutwaa ubingwa kwa msimu wa pili mfululizo tangu alipojiengua mwenyekiti wao Yusuf Manji

Dar es Salaam. Kitendo cha Simba kutwaa ubingwa kimepunguza msisimko kwa mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu yao inayocheza na Mbeya City kwenye Uwanja Uhuru jijini Dar es Salaam.

Mashabiki wa Yanga wachache wamejitokeza kwenye Uwanja wa Uhuru na kufanya mchezo huo dhidi Mbeya City kukosa shamla shamla ya vigoma kama ilivyozoeleka.

Mbali na kukosekana shamla shamla pia umakini wa baadhi ya mambo ni mdogo, Yanga inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Heritier Makambo dakika ya 27, lakini ubaoni wa matokeo hakuna anayeshugulisha na kubadilisha.

Kwa upande wa ushindani uwanjani Yanga ndio inaonekana kutawala mchezo zaidi kuliko Mbeya City ambao wanashambulia mara kwa mara.

Beki ya Mbeya City inaonekana kupambana kukabiliana na mashambulizi ya washambuliaji wa Yanga, wakiongozwa na Makambo, huku Papy Tshishimbi akicheza namba 10 anayocheza Ibrahim Ajib.

Pamoja na Tshishimbi hajazoeleka kucheza namba 10 lakini anaonekana kuimudu nafasi hiyo amekuwa akifika langoni kwa Mbeya City mara kwa mara.

Hali ya mvua inafanya uwanja kuwa na maji na kufanya wachezaji washindwe kuonyesha uwezo wao kwa asilimia 100 kutoka na mpira kushindwa kudundadunda kwa kukwama uwanjani.