Azam yapata ufadhili wa kuiua Lipuli fainali Kombe la FA

Muktasari:

GF Trucks inayojihusisha na uuzaji wa magari na vipuli vyake, ni miongoni mwa kampuni chache ambazo zimekuwa zikitoa udhamini katika soka Tanzania na hadi sasa inazidhamini timu za Alliance na Mbao FC za Mwanza.

Dar es Salaam.Maandalizi ya Azam FC kuelekea mchezo wa Fainali ya Kombe la Azam Sports Federation dhidi ya Lipuli FC utakaochezwa Juni Mosi, yamezidi kunoga baada ya timu hiyo kupata udhamini wa kampuni ya GF Trucks kwa ajili ya mechi hiyo.

Udhamini huo utahusu mechi ya fainali tu ambapo Azam FC itavaa jezi ambazo zitakuwa na nembo ya kampuni hiyo inayodhamini pia timu za Ligi Kuu Tanzania Bara za Mbao FC na Alliance za jijini Mwanza.

Mkataba huo umesainiwa jijini Dar es Salaam leo na kushuhudiwa na Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin 'Popat' na Mkurugenzi Mtendaji wa GF Trucks, Imrani Karmali huku wakishindwa kuweka wazi kiasi cha fedha ambacho klabu hiyo itapatiwa.

Akizungumza mara baada ya kusaini mkataba, Popat alisema kuwa ni kiashirio tosha kuwa klabu yake imefungua milango kwa kampuni na taasisi ambazo zinataka kuidhamini timu hiyo ambayo ni bingwa mtetezi wa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.

"Leo tumeingia mkataba na kampuni ya GF Trucks kwa ajili ya mechi yetu moja ya fainali ya Azam Sports Federation ambayo tunatarajia kwenda kuicheza Juni Mosi kule Lindi kwenye Uwanja wa Ilulu.Ni makubaliano tu ambayo sisi na wao tumekubaliana. Wao wameitaka kutudhamini katika mechi hiyo moja na sisi tumekaa tukakubaliana nao kwamba wao wataonekana pale juu ambako kulikuwa na nembo ya Tradegent.

Ni kwa pande zote mbili ambazo tutafaidika kwa sababu wao watajitangaza kupitia sisi na sisi pia tumepata udhamini tutajitangaza kupitia wao lakini pia ni njia nyingine ya kukuza urafiki baina ya wao na sisi.

Sisi Azam FC ni kampuni kama ilivyo kwa nyingine zote ambazo ziko kwenye biashara kwa hiyo kampuni yoyote ambayo iko tayari kuidhamini klabu yetu na ambayo inakidhi vigezo na mahitaji yetu tunaikaribisha na sio lazima iwe mdhamini mkuu bali inaweza kuwa mdhamini wa kawaida," alisema Popat.

Popat alisema udhamini huo sio lazima uwe wa fedha bali pia unaweza ukawa wa vitu na huduma.