Kagere aisaka rekodi ya miaka 20 ya Mmachinga

Muktasari:

Meddie Kagere anaongoza kwa kupachika mabao mengi msimu huu magoli 22 akifuatiwa na Salum Aiyee na Herieter Makambo wenye mabao 16 kila moja.

Dar es Salaam. Mabao 22 ya mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere imeanza kuitikisa rekodi ya miaka 20, iliyowekwa na nyota wa Yanga, Mohammed Hussein 'Machinga' aliyefunga magoli 26 katika msimu mmoja.

Mmachinga aliweka rekodi hiyo mwaka 1999, akifunga mabao 26, tangu wakati huo hakuna mchezaji aliyeifikia, lakini msimu huu Kagere akiwa amefunga mabao 22 anahitaji kufunga mabao manne katika mechi tatu zilizosalia za Simba kuifikia rekodi hiyo.

Kagere mbali ya kuisaka rekodi hiyo tayari mabao yake 22 yameivunja rekodi ya mshambuliaji wa Yanga, Amiss Tambwe aliyoweka msimu wa mwaka 2015/16 baada ya kufunga mabao 21.

Kwa kasi aliyonayo nyota huyo ya kupambana kupata mabao katika kila mchezo swali ni Je? anaweza kufikia rekodi ya Machinga na endapo atafikia rekodi hiyo basi ataandika ya kwake ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni kufunga mabao mengi zaidi.

Kagere kesho anatarajia kushuka uwanjani katika mchezo wa ligi dhidi ya Singida United ugenini endapo atapata nafasi ya kupachika mabao basi atakuwa anaisogelea rekodi hiyo ukiwa ni msimu wake wa kwanza kucheza Tanzania.

Hadi sasa rekodi ya nyota wa kigeni aliyefunga mabao mengi zaidi Ligi Kuu Tanzania Bara inashikiriwa na Tambwe aliyepachika mabao 21 na kufuatiwa na Emmanuel Okwi aliyefunga magoli 20 msimu uliopita.

Orodha ya wafungaji wa bora

1999- Mohammed Hussein 'Mmachinga' (Yanga) mabao 26

2005- Isse Abushir (Simba) mabao 19

2006- Abdallah Juma (Mtibwa Sugar) mabao 20

2007-08 Michael Katende (Kagera) mabao 11

2008-09 Boniface Ambani (Yanga) mabao 18,

2009-10 Mussa Mgosi (Simba) mabao 18

2010/11- Mrisho Ngassa (Azam) mabao 18

2011/12- John Bocco (Azam) mabao 19,

2012/13; Kipre Tchetche (Azam) mabao 17 

2013/14 - Amiss Tambwe (Simba) mabao 19 

2014/15- Simon Msuva (Yanga) mabao 17

2015/16 - Amis Tambwe (Yanga) mabao 21

2016/17- Simon Msuva (Yanga) na Abdulraham Mussa, mabao 14.

2017/18- Emmanuel Okwi (Simba) 20

2018/19- Meddie Kagere (Simba) 22 ligi inaendelea