Muktasari:

Simba inayohitaji kupata pointi tano tu ili iweze kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, ina mechi nne ikiwamo ya leo dhidi ya Ndanda ambazo inapaswa kuchanga vyema karata zake ili itetee taji lake la Ligi Kuu ambalo litaifanya iwe imelitwaa kwa mara ya 20 tangu klabu hiyo ilipoanzishwa.

Dar es Salaam. Hesabu za ubingwa na ugumu wa ratiba ya mechi tatu za ushindani zilizo mbele yao kabla ya kumaliza msimu, ni mambo mawili yanayoilazimisha Simba kushinda dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Uhuru leo jioni.

Ushindi kwa Simba utaifanya ifikishe pointi 88 ambazo zitakuwa ni moja pungufu ya pointi ambazo wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa, Yanga watazikusanya (89) ikiwa watashinda mechi zao mbili zilizobakia. Yanga wana pointi 83.

Simba inayohitaji kupata pointi tano tu ili iweze kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu, ina mechi nne ikiwamo ya leo dhidi ya Ndanda ambazo inapaswa kuchanga vyema karata zake ili itetee taji lake la Ligi Kuu ambalo litaifanya iwe imelitwaa kwa mara ya 20 tangu klabu hiyo ilipoanzishwa.

Lakini ili hesabu hizo za kusaka pointi tano za ubingwa zitimie, kuna ulazima kwa Simba kuhakikisha inaibuka na ushindi dhidi ya Ndanda ili ikwepe presha inayoweza kujitokeza kwenye mechi tatu zitakazofuata ambazo zinaonyesha wazi kuwa zitakuwa changamoto kwa Simba.

Mechi hizo tatu ni dhidi ya Biashara United ambayo Simba itacheza nyumbani na mbili za ugenini ambazo itakabiliana na Singida United na Mtibwa Sugar.

Ushindani mkali kwa Simba unatabiriwa kuwapo kwenye mechi zake dhidi ya Biashara United na Singida United kwani timu hizo kwa sasa zinapambana kukwepa kushuka daraja lakini mchezo dhidi ya Mtibwa ugenini, unaonekana unaweza kuwa mtihani kwa Simba kutokana na hali isiyoridhisha ya uwanja utakaotumika kwa mchezo huo ambao ni wa Jamhuri Morogoro lakini pia hamu ya wapinzani wao kulipa kisasi baada ya kuchapwa mabao 3-0.

Lakini pamoja na hilo, jambo gumu zaidi kwa Simba ni kwamba italazimika kucheza mechi hizo nne kuanzia ya leo pamoja na ile ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Sevilla ndani ya muda wa siku 10 na hivyo itakuwa ikipumzika kwa saa zisizozidi 48, muda ambao pia itatakiwa kuutumia kwa kusafiri kwenda mikoani na kurudi Dar es Salaam, hali inayoweza kuathiri ufanisi kutokana na uchovu kwa wachezaji wake.

Lakini kama itashinda leo, maana yake haitokuwa na presha wala kuhitajika kutumia nguvu kubwa kwenye mechi zake tatu za Ligi Kuu zitakazobakia kwani itakuwa ikihitaji pointi mbili tu ili itangazwe kuwa bingwa.

Simba inaingia kwenye mchezo huo ikijivunia rekodi ya kibabe iliyonayo dhidi ya Ndanda FC ambapo haijawahi kupoteza mechi yoyote dhidi ya timu hiyo ya Mtwara ambayo ilianza kushiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza msimu wa 2014/2015.

Katika michezo tisa iliyokutanisha timu hizo kwenye Ligi Kuu tangu Ndanda ilipopanda, Simba imeibuka na ushindi kwenye mechi nane huku mchezo mmoja ukimalizika kwa sare, ikifunga mabao 17 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara moja tu.

Matokeo pekee ambayo Ndanda inajivunia mbele ya Simba ni sare ya bila kufungana katika mechi iliyopita kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Kocha wa Simba, Patrick Aussems amesema anaamini watashinda leo dhidi ya Ndanda.