Yusuf Macho: Yule fundi wa mpira sasa kawa sangoma

ILIKUWA safari ya umbali wa saa kama mbili hivi kutoka Tabata Relini Mwananchi hadi Mbande ambako timu kamili ya Mwanaspoti ilitinga kwa kuzingatia maelekezo iliyopewa na gwiji wa soka nchini, Yusuph Macho ‘Musso’.

Huku ndiko yaliko maskani ya kiungo wa zamani wa Yanga, Simba, Mtibwa Sugar na Taifa Stars aliyekuwa na uwezo wa kuchezesha timu, kufunga na kuzuia, akitumia vyema mwili mkubwa ulioimarika kimazoezi hasa kwenye misuli ya paja na miguu. Ni wachache walifahamu kwamba jina lake halisi alilopewa na baba yake ni Macho.

“Jina langu ni Macho, baba yangu ni Yusuph na la ukoo ni Rwenda hivyo mimi ni Macho Yusuph Rwenda, lakini wengi walidhani jina langu ni Yusuph,” anasema Macho ambaye ni mwenyeji wa Mkoa wa Kigoma.

Macho amezaliwa katika Mtaa wa Bushabani, Kata ya Kibilizi, Kigoma. Alisoma Shule ya Msingi Buronge, Kigoma lakini kwa sasa, maisha yake ni Mbande jijini Dar es Salaam anakoishi pamoja na familia yake sambamba na kufanya shughuli zake.

Kama alivyomwelekeza mwandishi, baada ya kufika Mbande Mwisho ilipo stendi ya mabasi madogo, Macho alifika na kumpokea.

“Karibu dada, haya ndiyo maeneo yetu ya kujidai, mimi huku ni maarufu sana kutokana na kazi zetu kama kucheza mpira na nyingine,” anasema Macho.

Wakati anamkaribisha, kulikuwa sauti kubwa ikisikika kwenye spika ikikaribisha watu: “Karibu kwenye ofisi zetu, tunatibu magonjwa mbalimbali kwa dawa za mitishamba na kisunna. Tiba zetu ni nzuri kabisa.” Baada ya sauti hizo, Macho akasema: “Unasikia sauti hizo, hapo ni ofisini kwangu.”

AWA MGANGA WA KIENYEJI

Kumbe umaarufu aliokuwa nao hapo Mbande mwisho aliosema, mbali na kucheza soka, kwa sasa Macho ni mtabibu wa asili na anatibu kwa kutumia dawa za mitishamba na kisunna yaani zile za Kiarabu kwa jina lingine ni mganga wa kienyeji lakini mwenyewe anasema hapigi ramli.

“Mimi ni daktari si kama nakutania ni kweli kabisa (anaonyesha msisitizo na kuonyesha kitambulisho) natibu kabisa watu na wanajua kazi yangu,” anaeleza Macho.

“Sifichi ndiyo maana unaona spika hizo zinatangaza na ninajulikana katika umoja wetu kitambulisho changu ni hiki.” Baada ya mazungumzo hayo, Macho anasema: “karibu ofisini kwangu uone”.

MAMBO YA OFISINI KWAKE

Baada ya kufika ofisi hapo mwandishi alimkuta kijana mmoja akihudumia wateja waliokuwapo. Lakini, kitu cha kushangaza ni kwamba, baada ya Macho kuingia wateja waliongezeka kwa wingi, alikuwa mmoja lakini kwa mpigo waliingia kama watatu hivi. Mmoja alikuwa ni mama akasikika akisema: “Unaona tumbo langu linajaa tu.”

Macho akamjibu kwa kumwambia: “Pole sana mama, karibu upate tiba.”

Kwa ujumla hayo ndiyo maisha ya Macho katika kazi yake hiyo ya kutibu wagonjwa. Maisha mapya anayopitia baada ya kuwapiga chenga sana watu na kutupia mabao pale Uwanja wa Taifa.

ALIVYOINGIA KWENYE UGANGA

Macho ambaye mbali na duka hilo la Mbande ana jingine lililopo Mbagala anasema: “Niliijua elimu hii ya kutibu baada ya kumaliza darasa la saba. Badala ya kwenda sekondari nilikwenda kujifunza elimu ya dini ambayo niliisoma kwa takribani miaka mitano ndipo nikaingia kwenye mpira.”

“Katika elimu ile ya dini katika Chuo cha Ghazaal Muslim School pale Ujiji, Kigoma ambayo nilimaliza 1988, nilijifunza pia namna ya kusaidia watu, na pia kwenye familia yangu ni wataalamu, wanajua dawa,” anasema Macho ambaye kwa sasa ni Imamu wa Msikiti wa Masjid Adil, Mwembe Bamia, jijini Dar es Salaam.

“Upande wa mama yangu wako vizuri. Bibi yangu mzaa mama anatibu na pia mjomba wangu ni ‘fundi’ (mganga) tena fundi kwelikweli anaitwa Amri Ramadhani maarufu kwa jina la Abunuas.

“Huyu ni mjomba wangu kiukoo, alinifundisha dawa kipindi cha nyuma na baada ya kuachana na mpira, nilirudi tena nyumbani Kigoma akanifundisha kitalaamu kabisa,” anaeleza Macho.

ANASHIRIKIANA NA WENZAKE

“Natibu lakini tupo ushirika na madaktari wenzangu wengine, Dokta Kabora, Dokta Omary Mrisho, Dokta Babu Ally lakini pia katika ofisi zangu huwa naweka vijana kwa ajili ya uangalizi muda ambao nimetoka,” anasema Macho.

Anasema, anafanya kazi na madaktari wake hao kwa kushirikiana na ushauri: “Sisi tunatofautiana kitaalamu kuna mwenzangu unaweza kukuta ni mtaalamu wa kitu fulani na mimi nina ujuzi kwenye kitu kingine ambacho mwenzangu hajui.

“Anapotokea mgonjwa atatibiwa na mambo yanapomshinda mmoja wetu, mwingine kati yetu anaweza kuwa msaada katika hilo.”

TIBA ANAZOTOA

“Katika tiba zetu tunatibu matatizo yote ya binadamu. Tunatumia mitishamba na hizo za Kiarabu. Tunatibu vidonda vya tumbo, sukari, chango, kusafisha figo, kutoa sumu mwilini, uzazi, ganzi, maumivu ya viungo, kuvimbiwa na mengine mengi,” anasema Macho.

ENZI ZAKE ALIROGA WENZAKE?

“Kama unavyojua wakati nacheza mpira watu walikuwa wananiita Ustaadh na ndivyo nilivyokuwa. Nilikuwa mtu wa swala, nasoma vitabu vya dini, masahafu na kile cha majina 99 ya Mwenyezi Mungu. Binafsi nilikuwa muumini wa mazoezi, nilikuwa nafanya sana mazoezi kwa ajili ya kazi yangu ya mpira na kujitunza. Sikuwa najihusisha na mambo ya ushirikina, isipokuwa kuna dawa za kienyeji kama mafuta nilikuwa natumia kwa ajili ya kuchua na nyingine kutibu, unakunywa ni kama anti-bayotiki tu.”

Anaweka wazi mafuta aliyokuwa anatumia kujitibu yametengenezwa kwa nyonyo, nazi na karafuu.

“Maisha ya mpira kila mtu ana riziki yake kwa sababu mpira hauna ujanja. Binafsi nilikuwa mtu wa kusoma dua, natembea na msahafu, kitabu cha Majina ya Mwenyezi Mungu, mswala na tasbihi kwa ajili ya kuswali, lakini watu walipokuwa wananiona hivyo wakawa wananiogopa,” anasema Macho.

“Lakini, hivyo vitu ni vya kawaida, tasbihi kwetu ni sawa na ile rozari wanayovaa Waroma, ni vitu vya kiimani lakini watu walikuwa wananihofia kwelikweli walijua mimi kiboko.”

UCHAWI SIMBA, YANGA

Macho anasema, uchawi kwenye mpira hasa klabu za Simba na Yanga upo sana: “Wapo wachezaji wanaoamini bila kunawa dawa hawezi kufanya vizuri. Mtu anajua bila kutumia makombe (dawa inayoandikwa maandishi ya Kiarabu) kwa kunywa na kuogea hawezi kufunga bao.”

Anasema, kutokana na utaalamu na imani yake hakuwa anaamini jambo lakini watu walimwonya asifanye hivyo kwa sababu endapo timu inafanya vibaya wanasema yeye ndiyo amehujumu.

Anakumbuka mwaka fulani akiwa na moja ya klabu hizo kubwa walikwenda Bariadi Shinyanga na huko walifanya mambo mengi ya kutisha.

“Nakumbuka siku hiyo wachezaji hatukulala na binafsi nilibaki nacheka tu. Tulikuwa tunajiandaa kuikabili timu moja kubwa ya kimataifa, lakini kabla tulikuwa na mechi ya ligi kule,” anasema Macho.“Tulipelekwa kwa mganga mmoja ambaye karibu na nyumba yake kuna jiwe kubwa kama futi 13, sasa tukawa tunapanda juu tukifika kileleni tunashuka kwa kuserereka hadi chini, zoezi ambalo tulilifanya usiku kucha hadi kunakucha. Siku hiyo tulichoka sana,” anasema Macho na alipoulizwa kama mechi hiyo dhidi ya Shinyanga United walishinda, alikubali.

“Klabu moja niliyokuwapo wao walikuwa wakimtumia mama wa Kikongo ambaye yeye uchawi wake alikuwa anaweka kwa mtoto mchanga. Anakuja kambini na mtoto huyo na kufanya mambo yake, kwa hiyo ilikuwa kawaida tu. Timu nyingine ilikuwa kila mnapokwenda uwanjani gari la wazee watalaamu linatangulia mbele.”

Anasema, kikubwa ambacho alikuwa anafanya, anaacha mambo hayo yaendelee na yeye alijibidiisha kulinda kipaji chake kwa mazoezi na mambo mengine.

AWAPA DILI WACHEZAJI

Macho anasema, yeye harogi lakini ana dawa za kienyeji za kutibu majeraha ya mpira na hata ya kurogwa: “Anapokuja mgonjwa unamwangalia namna anavyoumwa, lakini si kwa kupiga ramli. Mimi sipigi ramli ni kutokana na anavyoumwa na dalili baada ya hapo unampa dawa ambazo unachanganya za magonjwa ya kawaida na kuvunja uchawi.”

“Tunampa dawa za kuchua kama mafuta na kunywa kwa mfumo wa dozi. mafuta ya kuchua sehemu zenye maumivu na ganzi baada ya muda mfupi maumivu yanapotea na nyingine za kuunga mifupa kama mchezaji amevunjika,” anasema Macho anayeweka wazi kuwa hata dawa za kupunguza uzito anazo.

MACHO NI NANI?

Macho ambaye alisoma Shule ya Msingi Buronge na alimaliza 1984, hakusoma elimu ya sekondari na badala yake alijikita kwenye elimu ya dini ya Kiislamu. Alisoma katika Chuo cha Ghazaal Muslim School kilicho Ujiji, Kigoma, elimu aliyoipata kwa kipindi cha miaka minne hadi 1988 na baada ya kumaliza ndipo akajikita kwenye soka rasmi. Anasema, 1989 alicheza mashindano ya Nzega, Tabora akiichezea Amka FC Ligi Daraja la Tatu mfadhili wao alikuwa NATCO Ahmad. Akiwa hapo alicheza kwa misimu miwili ya 1991 na 1992 akarudi kwao Kigoma mwaka ambao baba yake mzazi alifariki. Kwa sababu ya msiba alikaa Kigoma kwa muda akasaini Gungu Rangers na kuichezea kwa msimu mmoja.

AANZA KUCHEZA LIGI KUU

Anasema, mwaka 1994, akajiunga na Reli ya Morogoro wakati inacheza Ligi Daraja la Kwanza (Ligi Kuu sasa) ambako alimkuta Abeid Kasabalala, Mhammed Mtono, Gaspal Lupindo, Duncan Butinini, Boniface Njohole na Mathias Mulumba.“Kutokana na kiwango nilichokionyesha nikaitwa Klabu ya Waziri Mkuu Dodoma kwa ajili ya kuipandisha Ligi Daraja la Kwanza ambayo sasa ni Ligi Kuu tukafanikiwa kuipandisha,” anasema Macho.

Anasema, kutokana na kung’ara zaidi, Yanga walipata taarifa zake wakaweka nia ya kumsajili kipindi ambacho Sigara nao wakamsaka na kumsainisha.

Hivi unajua mambo aliyokutana nayo Musso alivyopata dili la kucheza soka la kulipwa kule England. Unafahamu ndoto zake zilikuwa kutua wapi? Hakikisha unaungana naye kesho hapa hapa, Mwanaspoti.