Pogba: Messi na Ronaldo wananiponza

Muktasari:

Mfaransa huyo, 26, anaamini kwamba mchango wake usingewekewa maswali na badala yake angesifiwa kama wasingekuwapo Lionel Messi wa Barcelona na Cristiano Ronaldo wa Juventus, ambao wanasababisha matarajio ya mashabiki kwa kila mchezaji yawe juu sana

Manchester, England. Paul Pogba amesema Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wanachangia lawama anazokumbana nazo mfululizo tangu arejee Manchester United.

Licha ya kutwaa Kombe la Dunia akiwa na timu yake ya taifa ya Ufaransa na kuwa mchezaji aliyethibitisha katika kiwango cha juu, kiungo huyo ameshuhudia mchango wake Old Trafford ukikosolewa daima.

Ameweka rekodi yake bora zaidi ya kufunga magoli msimu huu, akitupia mara 16 katika michuano yote.

Pogba pia ametoa ‘asisti’ 11, lakini hatima yake imezungukwa na uvumi mwiingi kutokana na kiwango chake.

Mfaransa huyo, 26, anaamini kwamba mchango wake usingewekewa maswali na badala yake angesifiwa kama wasingekuwapo Lionel Messi wa Barcelona na Cristiano Ronaldo wa Juventus, ambao wanasababisha matarajio ya mashabiki kwa kila mchezaji yawe juu sana.

Pogba aliliambia Jarida la Icon: “Soka limebadilika sana. Nilikua nikishuhudia utawala wa magwiji kama (Alessandro) Del Piero, (Luis) Figo, (Francesco) Totti na wengine wengi.

“Wote walikuwa ni washindi, wachezaji bora duniani, lakini bila ya shaka wengi wao hawakufunga zaidi ya magoli 20 kwa msimu.

“Messi na Ronaldo kwa wanayofanya – matarajio yamewekwa juu kuliko kawaida.”